Dar es Salaam. Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema atakuwa bega kwa bega na Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe katika mbio
zake za kuwania urais.
Membe, ambaye amekuwa akizungumzia kutangaza nia
kuwania urais kama “kusubiri kuoteshwa”, ameshasema siku ikifika
atachukua fomu lakini anatarajia kutangaza rasmi mpango wake jimboni
kwake Mtama, sasa anaungwa mkono na mmoja kati ya viongozi wa juu wa
Serikali na CCM kutoka Zanzibar ambayo ina nafasi ya pekee katika kuamua
mgombea urais wa chama hicho.
Balozi Iddi ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa
Mambo ya Nje tangu mwaka 2006, alitoa msimamo huo wa kwanza kwa kiongozi
wa juu wa Serikali jana jijini Dar es Salaam wakati akifunga mkutano wa
siku tatu wa mabalozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali, akimwakilisha
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein aliyeshindwa kuhudhuria kutokana
na msiba wa dada yake.
“Namtakia Membe safari njema na ninamuahidi kuwa
tutakuwa naye bega kwa bega katika safari hii ngumu kwake,” alisema
Balozi Idi bila ya kutaja neno urais.
Kauli ya makamu huyo wa Rais ilikuja baada ya
Membe, ambaye amesema wakati ukifika atachukua fomu za kugombea urais,
kuwaaga mabaozi hao kabla ya kumkaribisha mgeni huyo rasmi.
Katika hotuba yake ya mwisho kwa mabalozi hao,
Membe aliweka wazi kuwa hatarudi tena bungeni akiwa waziri baada ya
kuongoza wizara hiyo kwa takriban miaka minane.
Alirejea kauli yake ambayo amekuwa akiitoa mara
kwa mara kuwa ameamua kuondoka wizarani hapo ili kujaribu nafasi kubwa
zaidi katika siasa na kuwakaribisha bungeni mjini Dodoma ili wasikilize
hotuba ya bajeti yake ya mwisho.
“Njooni msikilize bajeti yangu ya mwisho kama
waziri kwani sitarajii tena kuingia bungeni kama waziri labda kwa nafasi
nyingine ambayo ni ngumu sana,” alisema Membe akiwaaga mabalozi 36.
Waziri huyo pia alitumia nafasi hiyo kuwaomba
mabalozi hao kuitangaza Tanzania nje, huku akitahadharisha kuhusu
mabadiliko ya kisiasa yanayoendelea kutokea katika baadhi ya mataifa
barani Afrika.
Alisema nchini Madagascar, Bunge limepiga kura ya
kutokuwa na imani na rais na kuilazimu Mahakama ya Katiba kufanya uamuzi
kuhusu suala hilo.
“Rais (Hery) Rajaonarimampianina amepigiwa kura
121 kati ya 125. Sitarajii kama kama Mahakama itaamua tofauti na matakwa
ya Bunge. Hukumu inatarajiwa kutolewa leo (jana) baada ya kura hizo
kupigwa jana (juzi),” alisema Waziri Membe.
Pamoja na kumuunga mkono Membe, Balozi Iddi
aliwataka mabalozi hao kutumia vyema nafasi walizonazo katika kuitangaza
Tanzania ili nchi inufaike na fursa za kiuchumi zilizopo huko walipo.
No comments:
Post a Comment