Thursday, 29 March 2018

Amuua mkewe na kuzika mwili wake

Na Gurian Adolf
Katavi.
Jeshi  la  Polisi mkoani Katavi  linamshikilia mkazi  wa  Kijiji  cha  Songambele  Kata ya  Sibwesa  Tarafa ya  Karema Wilaya ya  Tanganyika  jina  lake  limehifadhiwa(45) kwa  tuhuma za kumuua mke  wake(31) kwa sababu ya wivu wa kimapenzi na  kisha mzika huku  mtoto wake mwenye  umri wa miaka tisa akishuhudia tukio.
Kamanda wa  Jeshi la  Polisi wa  mkoa  wa  Katavi   Damas   Nyanda    alisema tukio  la kupatikana  kwa  mwili  wa  marehemu  huyo lilitokea juzi majira ya saa 6;00 mchana  katika Kijiji  hicho.
Alisema  kuwa  marehemu aliuawa  na  mumewe huyo siku ya  hapo  januari 15  kwa  kupigwa na  mumewe  kwa  kutumia silaha  zajadi ambazo ni fimbo na  mpini  wa   jembe baada ya  kumtuhumu kuwa  anamahusiano wa  kimapenzi na wanaume  wengine  Kijijini  hapo.
Kamanda   Nyanda alisema kuwa wakati mtuhumiwa  huyo akitenda kosa hilo   ambalo  lilishuhudiwa  na  mtoto  wake wa kiume hadi   baba  yake  alivyo muuawa  mama  yake  na  kisha  kushimba shimo na  kumfukia ardhini.
  Baada ya kufanya mauaji  hayo  na kuzika mwili huo mtuhumiwa alirejea  nyumbani  kwake na  kuendendelea  na  shughuli  zake  kama kawaida na  alimtishia  mtoto wake  huyo  mdogo na  kumwambia   asimwambie  mtu  yeyote.
Majirani  waliokuwa  wakimfahamu  marehemu  baada ya  kuona  haonekani  Kijijini  hapo walianza kumuuliza  mtuhumiwa  mahali  alipo  mkewe  naye   alikuwa  akiwajibu kuwa  mkewe  amesafiri kwenda kwao kusalimia.
 Kamanda huyo wa polisi  alisema kuwa Jeshi la  polisi  lilipata  taarifa   ya mauaji ya  mama  huyo  hapo  machi 15 na  ndipo  lilipoanza  uchunguzi wa  tukio  hilo.
Alileza  baada ya  kufanya  uchunguzi wa kina ndipo juzi   waliweza  kumtia  mbaroni  mtuhumiwa  na   baada ya  mahojiano  alikiri  kufanya  mauaji  hayo kwa  kile alichodai kuwa  alikasirishwa na  tabia ya  mke  wake ya kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanaume wengine kijijini  hapo  na  aliwaeleza  polisi kuwa  yuko  tayari  kwenda kuwaonyesha alipofukia mwili wa  mke  wake  baada  ya  kufanya mauaji.
Baada ya   mahojiano  hayo  hapo juzi  majira ya saa  6;00 mchana   polisi walifika  kwenye  eneo   ambalo  mtuhumiwa alikuwa  amemfukia  marehemu   mkewe na  baada ya kufukua  eneo  hilo walikuta  mwili na kuutambua kuwa ni mwili wa  mwanamke huyo na kisha kuutoa katika eneo hilo.
Kamanda   Nyanda  alisema kuwa  mwili   wa  marehemu baada ya kufukuliwa  ulichukuliwa na kupelekwa   katika   chumba  cha  kuhifadhi maiti katika  Manispaa ya  Mpanda.
Mtuhumiwa  anaendelea  kushikiliwa  na  jeshi la  polisi na  mara baada ya  upelelezi kukamilika  anatarajiwa kufikishwa  mahakamani  ili  akajibu  tuhuma zinazo  mkabili.
Mwisho

Thursday, 22 March 2018

Wafanyabiashara warejeshewa fedha zao

Na Gurian Adolf
Katavi

BAADA ya serikali mkoani Katavi kutoa siku saba kwa makampuni yaliyochukua fedha kutoka kwa wafanyabiashara kwaajili ya kuwauzia mashine za kulipia kodi za kielektroniki EFDs na hayakufanya hivyo,hatimaye makampuni hayo yamerudisha fedha hizo.

Akizungumza na gazeti hili katibu wa jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania,mkoani Katavi Robison Bumela alisema kuwa fedha hizo zimerejeshwa kwa wafanyabiashara waliopewa risiti kwakuwa walikuwa na vidhibiti.


Alisema kuwa wafanyabiashara wachache ambao hawajarejeshewa fedha zao ni wale waliokuwa wanalipia bila kupewa risiti na hivyo kuwa vigumu katika ushahidi ili kuwabana mawakala wa makampuni ambao walichuku fedha hizo.
Aidha katibu huyo alisema kuwa miongoni mwa changamoto zilizopo katika matumizi ya mashine za EFDs ni mashine hizo kutotunza kumbukumbu kwa muda mrefu hali inayosababisha kumbukumbu kupotea baada ya kufutika.
Kupitia mikutano mbalimbali ya wafanyabiashara,mkuu wa Mkoa wa Katavi Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga aliiagiza mamlaka ya ya mapato TRA Mkoani Katavi kuhakikisha wafanyabiashara wanarudishiwa fedha zao au wanakabidhiwa mashine EFDs ambazo walikuwa wamelipa fedha kwa mawakala kwakuwa walikuwa wakifanya kazi kwa kushirikiana na ofisi za TRA mkoa.
Mpaka mkuu wa mkoa huyo alipokuwa akitoa agizo hilo wafanyabiashara zaidi ya kumi walikuwa wakilalamikia kutapeliwa fedha na makampuni waliyoyalipa kwa madai kuwa yanauza mashine za EFDs lakini ilichukua miaka miwili bila kupatiwa mashine hizo.
Kwa mjibu wa wafanyabiashara Peter Mashinje mfanyabiashara wa mkoani humo alisema kuwa walikuwa wakilipia shilingi 800,000 lakini walipofanya malipo hayo na baadhi yao kupatiwa stakabadhi kimya kikawa kimetanda na hawakuelewa hatma ya fedha zao mpaka walipoamua kuieleza serikali ya mkoa huo kupitia vikao baina ya wafanyabishara na uongozi wa serikali ya mkoa.

Mwisho

Wanafunzi waugua ugonjwa wa ajabu

Na Gurian Adolf
Nkasi
WANAFUNZI wa kike wanaosoma katika Shule ya Msingi Kabwe  mwambao mwa Ziwa Tanganyika  wilayani Nkasi mkoani Rukwa wanaugua ugonjwa wa ajabu ambao unawasababisha kupiga kelele hovyo kutetemeka na kisha kuanguka.

Akizungumza na gazeti hili mkuu wa Shule hiyo , Amon Kawana alisema kuwa ugonjwa huo ulianza kutokea shuleni hapo tangu mwishoni mwa mwaka jana ambapo mpaka sasa ni wanafunzi wapatao 20 wa kike pekee ndio wanaougua ugonjwa huo na kusababisha taharuki  shuleni hapo.
“Tatizo hilo  lilianza mwezi Novemba mwaka jana ambapo watoto wa kike sita waliugua ugonjwa huo wa ajabu na ukaendelea na ilipofika mwezi Februari mwaka  huu  idadi imeongezeka kufikia 20… awali wakiugua tulikuwa tunawakimbiza  katika zahanati ya kijiji kwaajili ya matibabu ambapo ilibainika kuwa ni malaria kali lakini wakitibiwa baada ya muda mfupi wanaugua tena ugonjwa huo'' alisema
''hata hivyo  sasa ikitokea mwanafunzi kuugua ugonjwa huo tunawaita wazazi au walezi wao wanakuja  na  kuwachukua,nadhani wanawapeleka kwa waganga wa jadi kwakuwa wanaamini kuwa ni mapepo'' alisema mkuu huyo wa shule.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kabwe , Richard Madeni alisema  kuwa wachungaji  na waganga wa jadi wamekuwa wakiwashughulikia  tatizo hilo  bila mafanikio yoyote.
“Hivi Serikali ya Kijiji , walimu  na diwani  tumekutana na wazee maarufu baadhi yao ni waganga wa jadi waemdai tuwapatie siku mbili wajipange watatupatia jibu kesho pia tuandae ujira wao kabisa ili wamalize tatizo hili'' alisema.
Diwani wa Viti Maalumu , Christina Simbakavu alisema kuwa  tatizo hilo  limedumu kwa  muda mrefu na sasa limekuwa kero kwa  wazazi , walimu pia wakazi  wa kijiji hicho .
Kaimu afisa elimu msingi wilayani Nkasi Mnyuke Msumeno amekiri kuwapo kwa tatizo hilo na kuwa wamemuagiza mwalimu mkuu wa shule hiyo atoe taarifa ya maandishi itakayomfikia mkurugenzi mtendaji ili waone uwezekano wa kupeleka wataalamu wa afya katika eneo hilo.
Alisema kuwa tatizo hilo ni kubwa hasa kwa kuwa hutokea mara kwa mara hivyo wanaisubiri taarifa hiyo ili wataalamu wa afya waweze kwenda eneo la tukio ili waweze kuja na majibu ya tatizo lenyewe ikiwa ni pamoja na namna ya kulitatua.
Akizungumza na gazeti hili  kwa njia ya simu , Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Rukwa , Dkt Emanuel Mtika alisema kwa kuwa shule hiyo ni ya kutwa  na wasichana wanasumbuliwa  ni wenye umri chini ya miaka 16 na tayari  jitihada  kadhaa  ikiwemo wachungaji  kufanya maombezi  bila mafanikio  kuna uwezekano mkubwa  kuna mlipuko  wa ugonjwa wa malaria .
“Kijiji cha Kabwe (Nkasi ) hadi Kasanga (Kalambo ) ambavyo vipo katika ukanda  wa a mwambao mwa Ziwa Tanganyika  vimekuwa vikikumbwa na milipuko ya ugonjwa wa malaria ……wakazi wa maeneo hayo kutokana na hali ya joto  kali wamekuwa hawatumiii  vyandarua  usiku  hivyo kunauwezekano  mkubwa  kukawa na  mlipukjo wa ugonjwa wa malaria  katika kijiji cha Kabwe “ alisema Dkt Mtika .
Mwisho

Zambia yaondoa marufuku

Na Gurian Adolf
Kalambo

WAVUVI wa samaki katika ziwa Tanganyika wilayani Kalambo mkoani Rukwa wameishukuru serikali ya Zambia kwa kuondoa marufuku ya biashara ya samaki katika nchi hiyo ambayo ilikuwa imewekwa kwa takribani wiki mbili kutokata na kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa kipindu pindu nchini humo.
Shukrani hizo wamezitoa jana wakati wakizungumza na mwandishi wa habari wa gazeti hili ambapo walisema kuwa marufuku hiyo ilikuwa imewaathiri kiuchumi kutokana na kuwa soko kubwa la samaki wanaovuliwa katika ziwa Tanganyika wilayani Kalambo mkoani Rukwa nchini Tanzania ilikuwa ikitegemea soko katika nchi hiyo jirani.
Mmoja wa wavuvi hao ambaye ni mkazi wa Kasanga wilayani humo  aliyejitambulisha kwa jina la Richard Sichone alisema kuwa serikali ya nchi hiyo imeondoa marufuku hiyo baada ya jitihada za kukabiliana na ugonjwa huo kuonesha mafanikio ambapo hivi sasa wavuvi hao wameanza kuuza samaki wao nchini Zambia.
Alisema kuwa katika kipindi ambacho serikali ya nchi hiyo ilikuwa imezuia uvuvi katika nchi hiyo pamoja na biashara ya samaki kutoka nchi za Tanzania na Congo DRC kutokana na kipindu pindu walikabiliwa na ugumu wa maisha kwakuwa walikuwa wakiuza samaki kwa bei ya hasara tofauti na walipokuwa wakiuza nchini Zambia.

Sichone alisema kuwa katika nchi hiyo kuna makampuni 12 ambayo yamekuwa yakinunua samaki tani 1,200 kila siku ambapo kilo moja wavuvi wamekuwa wakiuza kwa shilingi 5,000 za kitanzania lakini katika kipindi ambacho nchi hiyo ilipiga marufuki ya biashara ya samaki soko lilishuka ambapo walikuwa wakiuza kilo moja kwa shilingi 1,500 na kulikuwa kuna kampuni moja tu ya Premji iliyopo Kasanga ambayo ilikuwa inauwezo wa kununua tani nane za samaki.
Naye Michael Sichilima mvuvi wa kijiji cha Kapele katika mwambao wa ziwa Tanganyika wilayani kalambo alisema kuwa kitendo ilichokifanya serikali ya Zambia ni chakupongezwa kwani kimetoa fursa ya biashara si tu kwa wavuvi wa nchini humo lakini pia wavuvi kutoka nchi jirani watanufaika.
Aliwasihi wavuvi kutoka mkoani wilayani humo kuheshimu sheria za nchi hiyo pindi wanapokwenda kufanya biashara ya samaki ili wasije kugeuka kero na kusababisha kuharibu uhusiano wa kibiashara na u dugu baina ya wanachi wa nchi hizo mbili kwakua mahusiano yao ni ya kihistoria na yanafaa kulindwa kwa maslahi ya waafrika wote.
Mwisho

Monday, 19 March 2018

Mbunge atoa vitendea kazi

Na Gurian Adolf
Sumbawanga

MBUNGE wa viti maalumu mkoani Rukwa(CCM) Silafu Maufi ametoa msaada wa vitendea kazi vya ofisi kwaajili ya jumuia ya Umoja wa wanawake mkoani Rukwa(UWT) ili viweze kuwasaidia katika kurahisisha kazi zinazo wakabili watendaji wa jumuia hiyo.

Akikabidhi vitendea kazi hivyo jana ambavyo  ni ngamizi (Computer) aina ya DELL pamoja na  kichapishi (printer) mbunge huyo alisema kuwa kabla ya kustaafu kazi na kuchaguliwa kuwa mbunge wa viti maalum alikuwa akifanya kazi ya Katibu wa CCM katika wilaya mbalimbali hapa nchini.
Alisema kuwa katika utendaji wake wa kazi alikuwa akikabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa vifaa kitendo kilichosababisha kutekeleza majukumu yake kwa shida na wakati mwingine kutokwenda sambamba na muda. 

Maufi aliwaeambia wanachama wa UWT kutoka wilaya za Kalambo, Nkasi, Sumbawanga mjini na Vijijini kuwa kumekuwa na tatizo la uvujaji wa siri za ofisi na za chama pia hasa katika kipindi cha chaguzi mbalimbali na sababu moja wapo ni kutumia ngamizi za nje ya ofisi kuchapa kazi za chama na jumuiya yenyewe.

Kutokana na changamoto hiyo ametumia kiasi cha shilingi milioni 10 kununua ngamizi nne pamoja na vichapishi aina ya HP vinne kila kimoja na ngamizi yake kwa ajili ya ofisi za UWT katika ofisi za wilaya zote katika mkoa wa Rukwa.


Kwaupande wake Beata Weller ambaye  ni katibu wa UWT wilaya ya Kalambo alitoa shukrani kwa niaba ya makatibu wengine ambapo alisema kuwa walikuwa wanalazimika kusafiri kilometa 50 kutoka Matai Kalambo kwenda mjini Sumbawanga kwaajili ya kuchapa kazi za jumuiya na kutumia gharama kubwa na wakati mwingine walilazimika kulala huko kutokana na kuwa ofisi yao ilikuwa haina vifaa hivyo muhimu vya kutendea kazi.

Alisema kuwa  licha ya kutoa shukrani za dhati kwa mbunge Maufi pia wanatoa pongezi kwa mbunge huyo kukumbuka alikotoka na kujaribu kutatua changamoto za kiofisi maana wabunge wengi wanawafikiria wananchi peke yao na kusahau chama na jumuia zake.

Chama cha Mapinduzi mkoani Rukwa kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa vya ofisi, ukosefu wa ofisi ambapo wilaya za Sumbawanga vijijini na Kalambo hazina ofisi kabisa.

Mwisho

Watoto wa kwenye mazingira magumu wawakera madiwani

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
BARAZA la madiwani la halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa limeviomba vyombo vya usalama vishirikiane na idaya ya uhamiaji  kuwakamata na kuwarudisha nchini kwao watoto wanaoishi katika mazingira magumu ambao wametoka katika nchi jirani za Zambia na  Congo DRC.
Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Justine Malisawa alisema hayo hivi karibuni wakati akiongoza kikao cha baraza hilo baada ya wajumbe kulalamikia kuongezeka kwa watoto ambao ambao wamekuwa kero na wanajihusisha na vitendo vya kihalifu ikiwemo uporaji.
Alisema kuwa hivi sasa mji wa Sumbawanga unakabiliwa na ongezeko la watoto wanaishi katika mazingira magumu ambao baadhi yao wanatoka katika nchi jirani ambao wamekuwa wakifanya vitendo vya kihalifu pamoja na ubakaji.
Malisawa alisema kuwa baada ya kubaini ongezeko la watoto hao halmashauri yake ilianza kuchukua hatua ambapo ilibaini baadhi ya watoto hao wanatoka katika nchi za Zambia na Congo DRC lakini baadhi yao wanatoka katika mikoa jirani na mkoa wa Rukwa.
‘’Ndugu zangu madiwani,hata mimi nakili kuwa watoto hawa ni bomu linalosubili kulipuka, baada ya jitihada za kuwafuatilia kujua tatizo ninini mpaka wanaongezeka kwa kasi kubwa tulibaini wengine wanatoka nchi jirani za Zambia na Congo DRC hivyo tunaomba vyombo vya usalama vishirikiane na idara ya uhamiaji warudishwe kwao’’ alisema.
Mmoja wa madiwani hao Vitalis Ulaya alisema kuwa watoto hao wanazidi kuongezeka kila kukicha katika mji wa Sumbawanga hali ambayo ni hatari kwakuwa hakuna jitihada za kutosha za kuweza kukabiliana na wimbi la ongezeko hilo.
Alisema kuwa wengi wa watoto hao wanazurula nyakati za mchana  wakiokota vitu majalalani na kuomba hela kwa wapiti njia na nyakati za usiku wamekuwa wakifanya vitendo vya uhalifu hali inayosababisha amani kutoweka.
Naye Ester Mpelele mjumbe wa baraza hilo alisema kuwa watoto hao wamekuwa ni changamoto kubwa kwa wanawake kwani hivi sasa huwezi kutembea pekeyako nyakati za jioni na usiku hali ambayo aliiomba serikali kuingilia kati jambo hilo.
Aliwaomba wazazi katika Manispaa hiyo ya Sumbawanga kuwajibika katika malezi ya watoto wao kwani kitendo cha kuwaacha bila kuwapa huduma za msingi ikiwemo elimu wanawaandalia maisha mabaya ya baadaye na watakuja kuisumbua jamii kutokana na kushindwa kuwajibika kwao.


Mwisho

Thursday, 15 March 2018

Walimu 16 watimuliwa kazi

Na Gurian Adolf
Nkasi

JUMLA ya walimu 16 wamefukuzwa kazi wilayani Nkasi mkoani Rukwa kwa kipindi cha miaka mitatu na wengine 11 wamepewa onyo kali baada ya kubainika wametenda makosa mbalimbali.

Katibu wa tume ya utumishi wa walimu TSC wilayani humo  Richard Katyega aliyasema hayo jana mbele ya kamishina wa tume ya Utumishi wa walimu Taifa, Samwel Koroso ambapo alisema  kuwa katika kipindi hicho  walipokea mashauri 23 na kupelekea walimu 16 kufukuzwa kazi,11 kupewa onyo kali na wengine 5 waliondolewa kazini baada ya kubainika kuwa na vyeti bandia.

Alisema kuwa  katika mwaka wa fedha wa 2016, 2017 na 18  tume hiyo imeweza kusikiliza mashauri hayo na kuyatolea maamuzi ambapo ilifikia maamuzi hayo baada ya kusikiliza mashauri hayo na pasipo kumuonea mwalimu hata mmoja na kutenda haki kwa mujibu wa sheria.

Katyega alisema kuwa tume hiyo sambamba na kuchukua maamuzi hayo pia imekua ikiwahamasisha walimu kufuata maadili ya ualimu kwa uhakika ili wasiweze kukumbana na adhabu mbalimbali ikiwemo kufukuzwa kazi kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake kamishna wa tume ya TSC Samwel Koroso alionyesha kusikitishwa na vitendo vya  uvunjifu wa maadili kwa waalimu hali inaoyopelekea  kufukuzwa kazi na kuwa wao kama tume ya maadili kwa walimu wataendelea kuwachukulia hatua Walimu wote ambao watakwenda kinyume na maadili ya ualimu

 Aliwataka walimu kwenda sambamba na misingi ya sheria ya utumishi kwa walimu kama inavyowataka na kuongeza kuwa walimu wilayani humo hawanabudi kuzipitia sheria za utumishi wa walimu ili waweze kuishi kwa kufuata sheria hizo zinavyo agiza.

Maofisa  kutoka ofisi ya ya kamishina wa tume hiyo nao waliweza kutoa mada mbalimbali zilizolenga kuwapatia elimu Walimu na kuwakumbusha sheria za utumishi wa walimu,huku walimu kwa upande wao walipata fursa ya kueleza changamoto zinazo wakabili  na zilipatiwa majibu kutokana na maswali waliyokuwa nayo.

Mwisho