Thursday, 22 March 2018

Wafanyabiashara warejeshewa fedha zao

Na Gurian Adolf
Katavi

BAADA ya serikali mkoani Katavi kutoa siku saba kwa makampuni yaliyochukua fedha kutoka kwa wafanyabiashara kwaajili ya kuwauzia mashine za kulipia kodi za kielektroniki EFDs na hayakufanya hivyo,hatimaye makampuni hayo yamerudisha fedha hizo.

Akizungumza na gazeti hili katibu wa jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania,mkoani Katavi Robison Bumela alisema kuwa fedha hizo zimerejeshwa kwa wafanyabiashara waliopewa risiti kwakuwa walikuwa na vidhibiti.


Alisema kuwa wafanyabiashara wachache ambao hawajarejeshewa fedha zao ni wale waliokuwa wanalipia bila kupewa risiti na hivyo kuwa vigumu katika ushahidi ili kuwabana mawakala wa makampuni ambao walichuku fedha hizo.
Aidha katibu huyo alisema kuwa miongoni mwa changamoto zilizopo katika matumizi ya mashine za EFDs ni mashine hizo kutotunza kumbukumbu kwa muda mrefu hali inayosababisha kumbukumbu kupotea baada ya kufutika.
Kupitia mikutano mbalimbali ya wafanyabiashara,mkuu wa Mkoa wa Katavi Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga aliiagiza mamlaka ya ya mapato TRA Mkoani Katavi kuhakikisha wafanyabiashara wanarudishiwa fedha zao au wanakabidhiwa mashine EFDs ambazo walikuwa wamelipa fedha kwa mawakala kwakuwa walikuwa wakifanya kazi kwa kushirikiana na ofisi za TRA mkoa.
Mpaka mkuu wa mkoa huyo alipokuwa akitoa agizo hilo wafanyabiashara zaidi ya kumi walikuwa wakilalamikia kutapeliwa fedha na makampuni waliyoyalipa kwa madai kuwa yanauza mashine za EFDs lakini ilichukua miaka miwili bila kupatiwa mashine hizo.
Kwa mjibu wa wafanyabiashara Peter Mashinje mfanyabiashara wa mkoani humo alisema kuwa walikuwa wakilipia shilingi 800,000 lakini walipofanya malipo hayo na baadhi yao kupatiwa stakabadhi kimya kikawa kimetanda na hawakuelewa hatma ya fedha zao mpaka walipoamua kuieleza serikali ya mkoa huo kupitia vikao baina ya wafanyabishara na uongozi wa serikali ya mkoa.

Mwisho

No comments:

Post a Comment