Thursday, 22 March 2018

Wanafunzi waugua ugonjwa wa ajabu

Na Gurian Adolf
Nkasi
WANAFUNZI wa kike wanaosoma katika Shule ya Msingi Kabwe  mwambao mwa Ziwa Tanganyika  wilayani Nkasi mkoani Rukwa wanaugua ugonjwa wa ajabu ambao unawasababisha kupiga kelele hovyo kutetemeka na kisha kuanguka.

Akizungumza na gazeti hili mkuu wa Shule hiyo , Amon Kawana alisema kuwa ugonjwa huo ulianza kutokea shuleni hapo tangu mwishoni mwa mwaka jana ambapo mpaka sasa ni wanafunzi wapatao 20 wa kike pekee ndio wanaougua ugonjwa huo na kusababisha taharuki  shuleni hapo.
“Tatizo hilo  lilianza mwezi Novemba mwaka jana ambapo watoto wa kike sita waliugua ugonjwa huo wa ajabu na ukaendelea na ilipofika mwezi Februari mwaka  huu  idadi imeongezeka kufikia 20… awali wakiugua tulikuwa tunawakimbiza  katika zahanati ya kijiji kwaajili ya matibabu ambapo ilibainika kuwa ni malaria kali lakini wakitibiwa baada ya muda mfupi wanaugua tena ugonjwa huo'' alisema
''hata hivyo  sasa ikitokea mwanafunzi kuugua ugonjwa huo tunawaita wazazi au walezi wao wanakuja  na  kuwachukua,nadhani wanawapeleka kwa waganga wa jadi kwakuwa wanaamini kuwa ni mapepo'' alisema mkuu huyo wa shule.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kabwe , Richard Madeni alisema  kuwa wachungaji  na waganga wa jadi wamekuwa wakiwashughulikia  tatizo hilo  bila mafanikio yoyote.
“Hivi Serikali ya Kijiji , walimu  na diwani  tumekutana na wazee maarufu baadhi yao ni waganga wa jadi waemdai tuwapatie siku mbili wajipange watatupatia jibu kesho pia tuandae ujira wao kabisa ili wamalize tatizo hili'' alisema.
Diwani wa Viti Maalumu , Christina Simbakavu alisema kuwa  tatizo hilo  limedumu kwa  muda mrefu na sasa limekuwa kero kwa  wazazi , walimu pia wakazi  wa kijiji hicho .
Kaimu afisa elimu msingi wilayani Nkasi Mnyuke Msumeno amekiri kuwapo kwa tatizo hilo na kuwa wamemuagiza mwalimu mkuu wa shule hiyo atoe taarifa ya maandishi itakayomfikia mkurugenzi mtendaji ili waone uwezekano wa kupeleka wataalamu wa afya katika eneo hilo.
Alisema kuwa tatizo hilo ni kubwa hasa kwa kuwa hutokea mara kwa mara hivyo wanaisubiri taarifa hiyo ili wataalamu wa afya waweze kwenda eneo la tukio ili waweze kuja na majibu ya tatizo lenyewe ikiwa ni pamoja na namna ya kulitatua.
Akizungumza na gazeti hili  kwa njia ya simu , Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Rukwa , Dkt Emanuel Mtika alisema kwa kuwa shule hiyo ni ya kutwa  na wasichana wanasumbuliwa  ni wenye umri chini ya miaka 16 na tayari  jitihada  kadhaa  ikiwemo wachungaji  kufanya maombezi  bila mafanikio  kuna uwezekano mkubwa  kuna mlipuko  wa ugonjwa wa malaria .
“Kijiji cha Kabwe (Nkasi ) hadi Kasanga (Kalambo ) ambavyo vipo katika ukanda  wa a mwambao mwa Ziwa Tanganyika  vimekuwa vikikumbwa na milipuko ya ugonjwa wa malaria ……wakazi wa maeneo hayo kutokana na hali ya joto  kali wamekuwa hawatumiii  vyandarua  usiku  hivyo kunauwezekano  mkubwa  kukawa na  mlipukjo wa ugonjwa wa malaria  katika kijiji cha Kabwe “ alisema Dkt Mtika .
Mwisho

No comments:

Post a Comment