Tuesday, 12 September 2017

Mazao ya poromoka bei Sumbawanga

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
Uingizwaji na uuzaji wa kinyemela wa Mahindi kutoka nchini Zambia, umetajwa umechangia kwa kiasi kikubwa kuporomosha bei ya soko la mahindi mkoani Rukwa.

Baadhi ya wafanyabiashara wa mazao hayo, waliopo katika soko la Mandela lililopo mjini hapa, walisema jana kwamba bei ya Mahindi  imeporomoka kwa kasi kubwa hali ambayo inawaathiri kibiashara.

Mmoja wa wafanyabiashara hayo, Josephat Maganga alisema kuwa bei ya mahindi kwa gunia moja imeshuka kutoka Sh 110,000 hadi Sh 42,000 hali ambayo imesababishwa na kukosekana kwa soko la mazao kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kuingiza nchini na kuuza mahindi kutoka nchi jirani ya Zambia.

"Wakati sisi haturuhusiwi kusafirisha mazao yetu na kuuza nchi jirani za  Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi na Rwanda ambako ndio lilikuwa soko letu la uhakika, sasa wenzetu wanaingiza mahindi kinyemela kutoka Zambia na kuuza hapa nchini.........hali inayosababisha soko  la bidhaa hiyo kushuka" alisema.

Alisema ipo haja sasa kwa serikali kuingilia kati na kudhibiti uingizwaji wa kinyemela wa mazao hayo kwa kuwa mkoa huo una ziada kubwa ya mahindi msimu huu.

Katika hatua nyingine, wafanyabiashara zao la Mbaazi nao walilalamikia kuporomoka kwa bei ya zao hilo kutoka Sh 78, 000 kwa gunia hadi Sh 30,000 hali ambayo inasababishwa na kukosekana kwa soko la bidhaa hiyo.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Tamson Simbowe alisema kuwa soko la mbaazi limeshuka kwa kasi kuliko ilivyokuwa mwaka jana, ambapo kilo moja walikuwa wakiuza kati Sh 100 hadi 800 lakini hivi sasa kilo moja uuzwa Sh 250.

Akizungumzia kushuka kwa bei ya Mbaazi afisa kilimo mkoa wa Rukwa, Hamza Mvano alisema soko la bidhaa hiyo lilikuwa nchini kenya ambako hivi sasa kumekuwa na uzalishaji mkubwa wa zao hilo hali ambayo imeathiri uuzaji wa zao hilo.
Mwisho

No comments:

Post a Comment