Na Gurian Adolf
Katavi
WALIMU wanne wa shule ya msingi Makongolo iliyopo katika Kata ya Magamba Manispaa ya Mpanda wanalazimkia kufundisha wanafunzi 380 kuanzia darasa la awali hadi la nne na wote wanafundishwa Katika vyumba viwili vya madarasa.
Mbali ya matatizo hayo shule hiyo pia ina matundu mawili ya vyoo kwa ajili ya wanafunzi huku walimu wakiwa hawana choo cha shule hivyo wanalazimika kutumia choo kilipocho katika nyumba ya mwalimu mkuu wa shule hiyo .
Akizungumza kwa sharti la kutoandika jina lake gazeti mmoja wa walimu wa shule hiyo ambayo iko umbali wa kilomita kumi kutoka mjini Mpanda alisema kuwa shule hiyo pia haina ofisi ya walimu ambapo wanalazimika kufanya shughuli zao chini ya miti.
“Najisikia vibaya sana kwenda kujisaidia kweny e choo kilichopo kwenye nyumba ya mwalimu mwenzetu kwa kuwa shule haina choo kwa ajili ya walimu…pia kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa ambavyo vipo viwili tu wanafunzi wanafundishwa kwa zamu"alisema mwalimu huyo.
Alisema kutokana na uhaba wa madarasa na uchache wa walimu wanalazimika wanafunzi wa shule hiyo kufundishwa kwa zamu huku wengine wakisomea chini ya miti.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Hosea Mpagasi akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea shule hiyo jana alisema kuwa shule hiyo ilianzishwa na kusajiliwa rasmi mwaka 2014.
“Shule hii inakabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu ambapo wapo walimu wanne tu hivyo mmoja wao akiugua au kupata dharura ina kuwa mzigo mkubwa kwa waliobakia “ alieleza.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Magamba Filipo Kalyalya alisema kuwa yeye kama mwakilishi wa wananchi katika kata hiyo hafurahishwi hata kidogo na changamoto hizo zinazoikabili shule hiyo huku akidai kuwa uongozi wa kata umekuwa ukichukua hatua mbalimbali ili kuinusuru shule hiyo lakini umekuwa ukikwamishwa na viongozi wa kijiji hicho .
Alisema kuwa Kampuni ya Ujenzi ya Kichina inayokarabati barabara inayounganisha Mji wa Mpanda na Kijiji cha Sitalike kwa kiwango cha lami ilitoa msaada wa matofali 400 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa lakini ni matofauli 40 tu yaliyofikishwa shuleni hapo huku mengine hayaeleweki yalipopelekwa na uongozi wa kijiji hicho.
“Nilipofuatilia Kampuni ya Ujenzi ya Kichina ilinithibitishia kuwa matofali yote 400 iliyotoa kama msaada kwa shule hiyo yalikabidhiwa uongozi wa kijiji cha Makongolo “ alisema diwani huyo .
Alisema kuwa atahakikisha kabla ya msimu wa mvua za masika kuanza Novemba mwaka huu ujenzi wa matundu ya vyoo vya wanafunzi wa shule hiyo vinaanza kujengwa ili kuwaepusha kukumbwa na magonjwa ya kuharisha ikiwemo kipindupindu.
Mwisho
No comments:
Post a Comment