Friday, 21 April 2017

Wafanyabiashara soko kuu kuendelea kufungiwa vyumba vyao vya biashara

Gurian  Adolf
Sumbawanga

BAADHI ya maduka ya wafanyabiashara katika soko kuu la mjini Sumbawanga huenda leo yakaendeleakufungwa baada ya mgambo wa halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga jana kuyafunga makufuli maduka yao kutokana na kushindwa kulipa bei mpya ya kodi ya pango.

Awali kabla ya mwezi februari mwaka huu halmashauri ya Manispaa hiyo ilikuwa inatoza vyumba vya biashara kodi ya shilingi 50,000 kwa mwezi kwa wapangaji wake ilioingia nao mkataba.

Akizungumza na rukwakwanza.blogspot.com mmoja wa wafanyabiashara katika soko hilo Frances Mayanga alisema kuwa wapangaji hao nao waliwatafuta wafanyabiashara na kisha kuwapangisha kwa bei ya juu zaidi hadi kufikia shilingi laki 3 kwa mwezi na hivyo kunufaika na vyumba hivyo.

Mwezi wa pili mwaka huu Manispaa iliamua kupandisha kodi ya vyumba katika soko hilo kutoka sh 50,000 hadi 120,000 na kisha kuwapa taarifa watu ilioingia nao mkataba.

Watu hao baada ya kupata bei hiyo mpya baadhi yao hawakuwaambia ukweli wafanyabiashara waliowapangisha na kuamua kukaa kimya wakiendelea kupokea fedha kutoka kwao bila kwenda kulipa kodi mpya katika ofisi za Manispaa.

Kutokana na manispaa kuwavumilia kwa muda sasa imeamua kuvifunga vyumba vya biashara ambavyo hawajatoa kodi mpya na waliojikuta wakiathirika ni wale waliopangishwa na watu walioingia mkataba na Manispaa.

Kutokana na hali hiyo Blogu hii iliamua kuwasiliana na mkurugenzi wa Manispaa hiyo Hamidu Njovu alisema kuwa msimamo wa Manispaa ni huo kuwa wanapaswa kulipa kodi hiyo mpya ya sh 120,000 hivyo wapeleke kodi hiyo ndipo watafunguliwa vyumba hivyo.

Alisema kuwa wao wanawatambua watu walioingia nao mkataba na wanataarifa za badiriko la kodi tangu mwezi wa pili sasa kama wameshindwa kuwasilisha fedha hizo warudishe vyumba hivyo ili Manispaa iwapangishe watu wanye uwezo wa kulipa kodi ya shilingi 120,000 kwa mwezi.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment