Sunday, 24 May 2015

RCC RUKWA YABARIKI JIMBO LA KWELA NA KALAMBO KUPIGWA PANGA

Na Gurian  Adolf
Sumbawanga

KAMATI ya ushauri ya mkoa wa Rukwa (RCC) jana imepokea na kuridhia maombi kutoka katika wilaya za Kalambo na Sumbawanga vijijini ya kutaka kugawa majimbo ya uchaguzi ya Kwela na Kalambo kutokana agizo la tume ya taifa ya uchaguzi NEC kutoa fursa ya kupokea maombi hayo na kuyakubali kama sababu zitakidhi haja.

Kikao hicho kilichoongozwa na mwenyekiti wake mkuu wa mkoa wa Rukwa Stella Manyanya kiliketi jana katika ukumbi wa mikutano uliopo katika jengo la ofisi ya mkuu wa mkoa na kuhudhuriwa na wajumbe wa kikao hicho.

Wakiwakilisha hoja ambazo tume itakubaliana nazo na kukubali kuligawa jimbo la Kwella na kupata jimbo jipya la Ziwa Rukwa kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga Linus Sikainda alisema kuwa jografia ya jimbo hilo inasababisha kuligawa jimbo la Kwela kwakuwa upande na mwingine umetenganishwa na bonde.

Alisema sababu nyingine inayosababisha kuligawa jimbo hilo ni idadi ya watu kwani jimbo ili ligawanywe ni lazima liwe na idadi ya watu wanaozidi 250,000 ambao wanasifa za kupiga kura idadi ambayo imezidi na iwapo jimbo hilo lisipogawanywa wakati huu fursa hiyo itatolewa na tume baada ya miaka 10 ambapo watu watakuwa wamezidi na kusababisha ugumu katika kutekeleza maendeleo jimboni humo.

Naye Kaimu mkurugenzi wa wilaya ya Kalambo Akilimali Mpozamenye alisema kuwa jimbo la Kalambo linastahili kugawanywa kutokana na kuwa idadi ya wakazi wake  imepungua kwa watu watano tu na kwamujibu wa sheria iwapo tume hiyo ikitoa fursa hiyo itakuja tena baada ya miaka 10 hali ambayo jimbo hilo litazidiwa na idadi ya watu kufikia wakati huo.

Alisema jimbo hilo ni kubwa kwa eneo na jografia yake ni ngumu hivyo ni bora likagawanywa na kupatikana jimbo la Mambwe ambalo litasababisha kufikiwa maendeleo kwa haraka kwani litakuwa ni eneo ambalo mbunge wake ataweza kulimudu ikiwa ni pamoja na fursa ya kuwafikia wananchi kwa urahisi.
Baada ya kuwasilisha hoja hizo na nyingine nao viongozi wa kisiasa ambao ni mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Rukwa Zeno Nkoswe akizungumza kwa niaba ya UKAWA alisema kuwa serikali ya mkoa inawajibu wa kutengeneza hoja nzito na zenye mashiko ili tume ya uchaguzi ya taifa ikubaliane nazo na kuyagawa majimbo hayo.

Naye Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa Rukwa ambaye pia alimwakilisha  mwenyekiti wa CCM, Clemence Bakuli aliwashukuru wajumbe hao wa RCC kwa kulikubalia hilo kwani alisema kuwa wametazama maslahi mapana ya mkoa ambapo kugawanywa kwa majimbo hayo kutaharakisha maendeleo katika mkoa huo.
Kwaupande wake mwenyekiti wa kikao hicho Manyanya alisema kuwa hii ni fursa pia kwa wanasiasa iwapo tume ya uchaguzi itayagawa majimbo hayo kwani ushindani utapungua kutokana na kuongezeka kwa majimbo mapya mawili.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment