Wednesday, 7 March 2018

wanafunzi 117 wajisaidia katika matundu mawili ya vyoo

Na Gurian Adolf
Kalambo

WANAFUNZI 117 wa kike wa shule ya sekondari Namema iliyopo kata ya Mambwekenya wilayani Kalambo mkoani Rukwa wanalazimika kujisaidia katika choo  chenye matundu mawili baada ya choo kilichokuwa cha wanafunzi kubomoka kutokana na kujengwa chini ya kiwango.

Akitoa taarifa jana kwa mkuu wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo,baada ya kufanya ziara shuleni hapo kaimu afisa elimu wa wilaya hiyo Saimon Mbwambo alisema kuwa ni takribani mwezi mmoja hivi sasa tangu choo hicho kibomoke  na kimesababisha usumbufu na kuleta hofu ya kutokea kwa magonjwa ya milipuko ikiwemo kipindu pindu kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Alisema kuwa halmashauri hiyo ilipokea fedha kutoka mradi wa SUPED kiasi cha shilingi milioni 233 ambapo ilitangaza zabuni na kampuni ya ujenzi ya Augo Company LTD ya jijini Dar es salaam na kushinda zabuni hiyo ambapo ilipewa kazi ya kujenga vyoo vya wavulana na wasichana,madarasa ,mawili pamoja na nyumba ya mwalimu.

Kampuni hiyo ilifanya kazi hiyo mwaka 2016 na kukamilika ambapo ilipwa fedha na zikawa zimebakia shilingi milioni 8.3 fedha ambazo ilikuwa bado haijamaliziwa ikiwa ni fedha za matazamio baada ya mradi kukamilika.

Ndani ya kipindi hicho cha matazamio kisichozidi mwaka mmoja changamoto zilianza kujitokeza ambacho choo cha wasichana kilitumbukia shimo lake na kwa upande wa choo cha wavulana kikaanza kutoa nyufa huku vyumba vya madarasa navyo vikatoa nyufa pamoja na sakafu kuchimbuka.

Kutokana na kubomoka kwa shimo la choo hicho cha wasichana kukasababisha hofu ya kukitumia yasije yakatokea madhara makubwa ikiwemo wanafunzi kutumbukia katika shimo hilo.

Akizungumzia hali hiyo Makamu mkuu wa shule hiyo Bahati Mswima alisema kuwa kutokana na hali ilivyo ilibidi busara itumike ambapo wanafunzi wa kike waliruhusiwa kutumia vyoo vya walimu ambavyo vinamatundu mawili ambayo hayakidhi mahitaji.

Alisema kuwa kwa upande wa wanafunzi wa kiume ambao idadi yao ni 199 wao wanatumia choo chao ambacho nacho huenda kikabomokea muda wowote kutokana na kutokuwa imara kwakuwa nacho kinaonekana kilijengwa chini ya kiwango.

Kaimu mkuu wa shule alisema kuwa kunahofu ya kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko kutokana na kuwa shulle hiyo kuwa na wanafunzi 316 ambao ni wengi na vyoo havitoshi baadhi ya wanafunzi wanalazimika kujisaidia porini kitendo ambacho ni hatari kwa afya zao.

Baada ya taarifa hiyo mkuu wa mkoa wa Rukwa Wangabo aliagiza mkandarasi aliyefanya ujenzi katika shule hiyo atafutwe na afikishwe shuleni hapo chini ya ulinzi ili afanye ukarabati haraka iwezekanavyo kwa fedha ambazo zimebakia na zisipotosha atumie gharama zake mwenyewe.

Alisema kuwa na tayari ameiagiza tasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU ifanye uchunguzi kuhusiana na kilichotokea na kuongeza kuwa hataki tena kuona kampuni hiyo inapewa kazi katika mkoa wa Rukwa.

Pia mkuu huyo wa mkoa aliwaijia juu watendaji wa halamshauri ya wilaya ya Kalambo kwakuwa walikuwa wanamshauri asifike kukagua shule hiyo ya sekondari kwamadai kuwa hawezi kufika kutokana na kuwa barabara ni mbaya na hakufikiki kirahisi.

''ndio maana mlikuwa hamtaki nifike shuleni hamkutaka nione madudu yaliyofanyika huku, watendaji wa serikali inawapasa mbadirike, muwe na uchungu na mali za serikali namna hii hatuwezi kwenda'' alisema.

Aidha mkuu huyo wa mkoa aliwaasa wanafunzi wa shule hiyo kusoma kwa bidii na serikali itatatua changamoto iliyojitokeza ndani ya muda mfupi wanachotakiwa ni kuongeza bidii katika masomo yao.

Mwisho

No comments:

Post a Comment