Na Israel Mwaisaka
Nkasi
WAZEE wilayani Nkasi mkoani Rukwa wamemshauri rais Dk,John Magufuli asilegeze uzi katika jitihada za kulinda rasilimali za taifa na kutetea wanyonge kwani watanzania walimchagua wakiamini Kuwa anaweza kazi hiyo.
Wakizungumza Jana kupitia risala yao mbele ya mkuu wa wilaya Nkasi aliyewakilishwa na katibu tawala wa wilaya hiyo Festo Chonya kwenye maadhimisho ya siku ya wazee duniani walisema kuwa jitihada zinazofanywa na rais Magufuli ni za kuungwa mkono na kila mtanzania mpenda maendeleo.
Akisoma risala hiyo katibu wa umoja wa Wazee wilayani Nkasi Said Juma alisema kuwa wao wakiwa ni wazee ndiyo wanafahamu vizuri nchi hii ilikotoka na ilipofikia hivi sasa na kumsihi raisi asikubali kuyumbishwa nawatu wachache ambao ni vibaraka wa mataifa mengine wanaopenda kuinyonya nchi yetu na watanzania kubaki kuendelea Kuwa masikini.
Alisema tangu enzi za ukoloni wananchi hawajanufaika vya kutosha na rasilimali zao kutokana na baadhi ya viongozi wachache ambao wamekuwa wakijali maslahi yao binafsi Lakini hivi sasa amepatikana rais mzalendo ambaye anania ya kulisaidia taifa.
Aidha alitumia nafasi hiyo kuiomba serikali kuanza kuwapa Pensheni Wazee wote waliofikisha umri wa miaka 60 ili kuweza kurahisisha maisha yao kutokana na changamoto nyingi wanazikabiliana nazo kwani licha ya kwamba baadhi yao hawakuwa waajiriwa serikali Lakini wanamchango mkubwa katika nchi tangu enzi za kupigania uhuru, vita ya Kagera na katika vipindi mbalimbali ambavyo nchi ilipitia changamoto.
Alisema hivi sasa serikali inatoa pensheni kwa wazee waliofanya kazi serikalini pekee lakini sasa ni wakati wa kuwaangalia wazee wote waliofikisha umri huo kuweza kupewa pensheni kwani nao wameshiriki kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa taifa hili.
Waliishukuru serikali kwa kulipa kipaumbele suala la matibabu bure kwa Wazee na kuitaka serikali kuongeza jitihada katika eneo hilo ili Wazee wote waweze kupata vitambulisho vitakavyowasaidia wao kuweza kuyapata matibabu bure kama sera ya wazee inavyosema.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya aliyewakilishwa na katibu tawala wa wilaya Festo Chonya aliwataka Wazee kuwa na subira wakati serikali ikiendelea na mchakato juu ya pensheni zao,huku akidai kuwa sasa vitambulisho vya Wazee vitapatikana kwa wakati ili waendelee kupata matibabuya bure.
Alisema wilaya Nkasi pekee ina wazee wapatao 18,000 wanaohitaji vitambulisho na vilivyopo sasa ni 4000 tu na kuwa kufikia mwakani watajitahidi kuona wazee wote wanapata vitambulisho hivyo.
Naye kaimu mganga mkuu wa wilaya Nkasi Juliana Namfukwe alisema kuwa mpaka sasa wametenga shilingi milioni 6 zitakazotumika kutengenezea vitambulisho vya Wazee wilayani humo.
Kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya Abel Ntupwa alisema kuwa wao kama halmashauri wanajitahidi kutekeleza Sera za Wazee na kuwa baadhi ya changamoto wamekua wakijitahidi kuzitatua na lengo ni kutaka kuona Wazee wanaishi maisha bora zaidi.
Siku ya Wazee Duniani wilayani Nkasi imeadhimishwa kwa Maandamano ikiwa ni pamoja na kupimwa afya zao hususani kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Maadhimisho ya siku ya Wazee mwaka huu yamebeba ujumbe usemao “Kuelekea Uchumi wa viwanda ,Tutathmini changamoto ,Uzoefu na ushiri wa Wazee kwa maendeleo ya taifa.
Mwisho
No comments:
Post a Comment