Na Gurian Adolf
Katavi
Madiwani wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi wamempongeza rais John Magufuli kwa ujasiri aliouonesha wa kulinda rasilimali za nchi hasa katika suala la madini na pia wamelaani vikali baadhi ya watu wanaobeza jitihada alizozifanya.
Pongezi hizo kwa rais walizitoa jana kupitia waandishi wa habari ambapo Meya wa Manispaa ya Mpanda Willy Mbogo alizungumza niaba ya madiwani hao.
Alisema madiwani wa Manipaa ya Mpanda wameamua kutoa tamko mahsusi la kumpongeza rais Magufuli kwa ujasiri aliouonesha wa kulinda rasilimali za nchi hasa katika suala zima la madini.
Mbogo alisema wanawalaani vikari baadhi ya watu ambao wanaobeza jitihada zinazofanywa na rais za kulinda rasilimali zetu za nchi nahasa madini kwa ajiri ya manufaa ya Watanzania wote.
"Rais mwanzo aliunda kamati mbili ambazo zilitoa taarifa na sasa amefanyia kazi mapendekezo yaliotolewa na kamati hizo na tayari tumeanza kupata manufaa makubwa kwani Kampuni ya Barick Gold imekubali kutupa asilimia 16 ya hisa za kampuni hiyo",alisema
"Pia wamekubali kulipa Dola za kimarekani milioni mia tatu na kugawana nusu kwa nusu faida ya mapato yanayopatikana,kitu ambacho kimetokana na jitihada za rais wetu za kulinda rasilimali za nchi yetu"
Alisema madiwani wa Manispaa ya Mpanda wanaamini mapato hayo yatakayopatikana yataongezeka Serikali na halmashauri zote zitaongeza uwezo wa kuwahudumia wananchi.
Naye diwani wa Kata ya makanyagio Haidari Sumry aliomba jitihada za rais zisiishie kwenye madini tu bali nguvu iongezeke kwenye maeneo mengine ili uchumi wa nchi uweze kukua na kuongezeka zaidi ya hivi sasa.
Alisema endapo rasilimali za nchi zitasimamiwa vizuri halmashauri zitanufaika na mapato yataongezeka Serikalini kwani hata huduma kwenye halmashauri zitaboreshwa zaidi.
Kwaupande wake diwani wa viti maalumu katika halmashauri hiyo Getruda Kabinda alisema kuwa watu ambao walikuwa wakinufaika peke yao na rasilimali za nchi hii ndio wanaobeza na kupinga jitihada zinazofanywa na rais kwa manufaa ya watanzania wengi katika kulinda rasilimali za nchi.
Alimuomba rais Magufuli kukaza uzi kwani watanzania wanyonge wanatambua anachokifanya na kamwe asikatishwe tamaa na wasaliti wachache kwa maslahi yao,kwani hatua anazochukua japo siku moja atakufa lakini atabaki anaishi katika mioyo ya wanyonge Kama baba wa taifa mwalimu Julius Nyerere.
Mwisho
No comments:
Post a Comment