Na Gurian Adolf
Sumbawanga
BAADHI
ya wanawake wa kata ya Lyangalile wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa
wamelalamikia kitendo cha kutozwa fedha kiasi cha shilingi 50,000 kama adhabu kutokana na kujifungua katika eneo ambalo si salama na hakuna
huduma za uzazi salama.
Wanawake hao walitoa malalamiko yao kwa
Katibu wa CCM mkoa wa Rukwa Mwanamasudi Msafiri Ibrahim Pazi alipokuwa
katika kata hiyo akifanya ziara ya kukagua maendeleo ya chaguzi za ndani
ya chama hicho na kusikiliza changamoto walizonazo wakazi wa kata hiyo.
Wakizungumza
kwa malalamiko
wanawake hao walisema kuwa wamekuwa wakitozwa fedha hizo na watendaji
wa afya pindi wanapofika katika vituo vya uzazi salama kwa lengo la
kupata matibabu.
Mmoja
wa wanawake hao aliyejitambulisha kwa jina la Marystella Kaputa mkazi
wa kata hiyo alisema kuwa wanaumia sana kwa kitendo cha kutozwa fedha
hizo kama faini kutokana na kutojifungulia katika eneo ambalo halitoi
huduma za uzazi salama kama majumbani na njiani wanapokuwa wanapelekwa
kujifungua.
Alisema
kuwa inawezekana nia ni njema ili kuwaadhibu wanawake ambao hawaendi
kujifungua katika vituo vya huduma za uzazi salama lakini adhabu hiyo
imekuwa ni kubwa sana hasa ikizingatiwa kuwa sio wote wanaofanya hivyo
kwa makusudi bali wengine wanajikuta inawatokea kutokana na changamoto
mbalimbali ikiwemo ni pamoja na usafiri, maandalizi duni sambamba na
ndugu zao kutofanya maamuzi wakati uchungu unapo waanza.
Naye
Adelina Severino mkazi wa kata hiyo alisema kuwa kitendo wanachofanyiwa
wanawake hao sio sawa bali kinachotakiwa ni watendaji wa afya
kuendelea kutoa elimu ili wanawake waone umuhimu wa kwenda kujifungulia
katika maeneo yanayotoa huduma za uzazi salama kama zahanati, vituo vya
afya na hospitali ili kuepuka changamoto zinazoweza kuwakuta wakati
wakijifungua katika maeneo hayo.
Kwa
upande wake Sekunde Nanyumbu mkazi wa kata hiyo alisema kuwa wakati
mwingine wanawake wanakutwa na hali hiyo kutokana na ndugu wa karibu
kama mume, wakwe na wengine wenye maamuzi katika ukoo kutowaruhusu
ama kufanya maamuzi ya haraka ili wafike katika maeneo yanayotoa huduma
za uzazi salama na katika kata hiyo wanategemea zahanati iliyopo katika
kijiji cha Katonto ambapo baadhi yao wanaishi umbali wa kilometa nne
mpaka kuifikia zahanati hiyo hali ambayo imekuwa ikichangia wanawake
kujifungua katika maeneo ambayo siyo salama kwao.
Hata
hivyo katibu huyo wa ccm mkoa wa Rukwa alilaani kitendo hicho na
kuahidi malalamiko yao kuyafikisha kwa watendaji wa afya ngazi ya mkoa
ili yashughurikiwe na kukomeshwa kabisa kwani mpaka sasa Sera ya afya
ni huduma bure kwa wakina mama wajawazito kitendo cha kuwa toza faini
siyo sawa.
Baada
ya rukwakwanza.blogspot.com kupata malalamiko hayo iliwasiliana na kaimu mganga
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Emmanuel Mtika alikiri kuwepo kwa malalamiko hayo
na kusema kuwa wanaopaswa kupewa adhabu ni wanawake wanaojifungulia
nyumbani ili waache tabia hiyo na si wale wanao jifungulia njiani lakini pia alisema tume imeundwa
kwa lengo la kuchunguza malalamiko hayo ili hatua ziweze kuchukuliwa
kwani ni kosa kuwatoza faini hiyo ya shilingi 50,000 ambayo ni kubwa.
Mwisho
No comments:
Post a Comment