Tuesday, 17 December 2013

MVUA YASABABISHA KAYA 32 KUKOSA MAKAZI RUKWA


ZAIDI ya kaya 32 zimebaki makazi ya kuishi katika kijiji cha
Kasense nje kidogo ya mji wa Sumbawanga baada ya mvua kubwa
iliyoambatana  na upepo mkali kunyesha kwa  takribani masaa mawili na
kusababisha uharibifu mkubwa.

Mvua hiyo ilianza majira ya saa 10;15 huku kukiwa na upepo aina ya
kimbunga  ilinyesha mpaka majira ya saa  12;00 huku ikisababisha
kuezua paa ya baadhi ya nyumba kijijini hapo nyumba nyingine
zikibomoka kabisa na kuzua tafrani ya hari ya juu kwa wakazi wa kijiji
hicho.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho Fafael Simuyemba alisema kuwa kabla ya
kuanza kunyesha mvua hiyo lilitamba wingu jeusi ambalo hawajawahi
kuliona na kisha ulianza kuvuma upepo mkali ulianza kusababisha
madhara madogo madogo.

Kutokana na muda ulivyozidi kwenda yalianza manyunyu ya mvua na kisha
mvua kubwa kunyesha licha ya kwamba ilikuwa ni jioni lakini giza
lilitanda na watu wakawa hawana la kufanya isipokuwa kujikuta wakilia
na kuomba Mungu kwani baadhi yao walijua ni mwisho wa dunia.

‘’Huwezi kuamini ndugu mwandishi hata sisi wanaume watu wazima
tuliingiwa na hofu tukapoteza ushujaa na kujikuta tukilia tukiamini
huenda ndiyo mwisho wa dunia ambao huwa wanausema maana mimi sijawahi
kuona kitu kama kile’’…alisema Simuyemba.
Naye Joyce Kalicha mkazi wa kijiji hicho alisema taabu ilikuwa kwa
wanawake maana walikosa wakimbilie wapi maana wengine wana watoto
wadogo kwani mvua ilikuwa ni kubwa kupita kiasi hata kwenda kwa jirani
yako haiwezekani.

Alisema kuwa baadhi ya watu walikuwa wakiangukiwa na matofali ya
nyumba zao lakini hakuna aliyepoteza maisha wala kupatwa na jeraha
kubwa isipokuwa nyumba kuezuliwa na nyingine zikianguka kabisa huku
baadhi ya mali kuharibika vibaya.

Baada ya mvua hizo kukatika na kupata taarifa ya maafa hayo mkurugenzi
wa halmashauri ya Sumbawanga William  Shimwela  alifika katika kijiji
hicho akiwa na timu ya watendaji wa halmashauri hiyo ambapo aliwapa
pole wananchi hao kisha kuwaomba wasaidiane katika mahitaji mbalimbali
kwakuwa baadhi yao walikuwa hawana hata sehemu ya kuishi.

Alisema kuwa Halmashauri imeona hali hiyo na inafanya tathmini na
ndani ya muda mfupi watapata misaada mbalimbali ambayo itawawezesha
kurejea katika hali zao kutokana na uharibifu mkubwa uliotokana na
mvua iliyonyesha kijijini hapo.

No comments:

Post a Comment