Na Walter Mguluchuma
Katavi
Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi limewaua majambazi wanne wakiwa na Bunduki mbili za kivita zikiwa na risasi 27 baada ya majibizano ya risasi na Polisi yaliyochukua muda wa dakika kumi na tano.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Benedictor Mapujila alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa tano usiku katika eneo la Kahenze Kata ya Ugala Tarafa ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi.
Alisema kuwa siku moja kabla ya kuuawa kwa majambazi hayo majambazi yalimpora mtu mmoja aliyefahamika kwa jina Shija Masanja ambae alikuwa ni mfanyabiashara walimvamia huku wakiwa na silaha na waliweza kumpora simu mbili aina ya TECNO na pesa tasilimu Tshs 800,000 na kisha kutokomea kusiko julikana.
Kaimu Kamanda Mapujila alisema jeshi la polisi lilipata taarifa za tukio hilo na ndipo walipoanza msako mkali wa kuwasaka majambazi hao katika maeneo ya Kata nzima ya Ugala.
Alisema katika msako huo Polisi waliweza kuwaona majambazi hao wakiwa wamejificha kichakani kando ya barabara na baada ya kuona wanafuatwa na askari majambazi hao walianza kuwafyatulia risasi askari polisi huku wakikimbia wakielekea kichakani.
Katika majibizano hayo ya risasi yaliodumu kwa muda wa dakika 15 polisi walifanikiwa kuwaua majambazi wanne na kuwakuta wakiwa na silaha mbili Bunduki za kivita aina ya SMG zenye Namba za usajili UA 5538 1997 ikiwa na risasi 14 kwenye magazine na nyingine yenye namba AFV 0826 1996 ikiwa na risasi 13 kwenye magazine.
Mapujila alisema majina ya majambazi hao yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi na miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda.
Kaimu Kamanda ametoa wito kwa wananchi wale wanaomiliki silaha kinyume na utaratibu kuzisalimisha silaha hizo mara moja kwani Jeshi la polisi halitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakae bainika kumiliki silaha kinyume cha sheria.
Mwisho
No comments:
Post a Comment