Thursday, 27 July 2017

Mimba za utotoni janga la kiwilaya Nkasi

Na Israel Mwaisaka
 Nkasi .
SERIKALI ya Wilaya ya Nkasi  mkoani Rukwa imetangaza  rasmi  kuwa tatizo la  mimba na ndoa za utotoni  ambalo limesababisha wanafunzi wa kike kukatiza masomo yao  katika shule za msingi na sekondari ni janga la wilaya huku ikitangaza vita kali dhidi yake .
Kauli hiyo ilitolewa  na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi , Julius Kaondo baada ya madiwani wa halmshauri hiyo wakiitaka Serikali  ichukue hatua  kali dhidi  ya wote wanaohusika katika  kukatiza  masomo ya wanafunzi wa kike  kwa  kuwapatia ujauzito wanafunzi na  kuwaoa  wakiwa bado wadogo .
Kaondo alibainisha kuwa  tayari opereshini maalumu ya kuwasaka  wazazi , watendaji , walimu wakuu  na wanaume wanaoshirikiana kumaliza  mashauri ya mimba shuleni na ndoa za utotoni  kwa siri ili waweze kuozeshwa kwa malipo ya mahari kubwa .
“Ili kuhakikisha  na kuimarisha opereshini hiyo maalumu tayari  Ofisi ya DED  imempatia  mafuta ya kutosha  Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Nkasi (OCD ili ayatumie katika gari  litakalotumika katika  opereshini hiyo  maalumu “ alisisitiza .
Akizungumza na gazeti hili OCD wa Nkasi , David Mtasya  kabla  ya kuanza kwa operesheni hiyo maalumu alibainisha kuwa tayari Maofisa Watendaji  kutoka Kata Sita wilayani humo wanashikiliwa  na Jeshi la Polisi wakituhumiwa kuhusika na  kumaliza  kesi za mimba shuleni kwa siri nje ya mahakama ambapo wazazi  na watuhumiwa  wanakubalina  kunapatana  na kuiozeshwa watoto hao  baada ya kulipa mahari .
Mwisho 

No comments:

Post a Comment