Monday, 5 June 2017

Njovu awaasa kulipa kodi

Na Gurian  Adolf
Sumbawanga

HALMASHAURI ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa imewataka wakazi  wa Manispaa hiyo kuhakikisha kuwa wanalipa kodi  za aina mbalimbali ikiwemo kodi ya mashamba, nyumba na viwanja kwa wakati ili kuepuka mkono wa sheria sambamba na kunyang'anywa baadhi ya vitu na mali wanavyodaiwa kodi  kwakua kutokuvilipia ni kosa kisheria.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Hamid Njovu alisema hayo wakati akizungumza na rukwakwanza.blogspot ilipotaka kujua muitikio wa wananchi katika kulipa kodi  mbalimbali ambazo wanapaswa kulipa kisheria ili waiwezeshe halmashauri hiyo na serikali kukuu kupata mapato kwaajili ya utekelezaji wa bajeti za serikali.

Alisema kuwa bado kuna  mwamko mdogo wa ulipaji kodi  na ushuru kwa hiari kwa baadhi ya wananchi wa Manispaa hiyo wamezoea kulipa kwa kubanwa hadi kuchukuliwa hatua za kisheria kitu ambacho siyo sawa wanapaswa kubadirika vinginevyo itawagharimu kwani hivi sasa serikali haina masihara katika kukusanya mapato.

Mmoja wa wakazi wa mji huo wa Sumbawanga Anatory Sikulumbwe alisema kuwa ni vizuri kwa serikali kuu  na halmashauri kuhakikisha pia zinawatendea haki  wananchi kwa kuwapimia ardhi, kuwapa hati za viwanja na hati miriki za ardhi na mashamba  ili waweze kunufaika kwa kupata mikopo katika mabenki wakitumia Mali hizo kama dhamana.

Naye  Maria Kaswaya alisema kuwa wengi  wa wananchi katika mji huo wanamiriki nyumba na ardhi ambazo hazijapimwa na hivyo kushindwa kunufaika nazo  pindi wanapotaka kuzitumia kama dhamana katika tasisi zinazokopesha kwakua hazijapimwa na kurasimishwa.

Alisema kuwa wapo wanawake ambao ni masikini wa kutupa  kwa kukosa mitaji lakini wanamiriki mashamba  na nyumba lakini zinakosa dhamani na hazifai kama dhamana kutokana na kuwa zipo katika maeneo ambayo hayajapimwa na hazina  hata hati miliki.

Kaswaya aliuomba uongozi wa halmashauri hiyo kulitazama suala hilo kwa umakini ili wanawake hao na makundi mengine  waweze kunufaika na rasilimali walizonazo na kujikomboa kutoka katika umasikini.

Mwisho

No comments:

Post a Comment