Na Gurian Adolf
Sumbawanga
MTU mmoja anayefahamika kwa jina la Fokas Pera(48) mkazi wa kitongoji cha Ilemba B, kata ya Nankanga tarafa ya Laela wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa ameuawa na rafiki yake kwa kumkata na kitu chenye ncha kali kinachodhaniwa kuwa ni panga kichwani kwa madai kuwa alimdhurumu mbao mbili.
Tukio la mauaji hayo kilitokea Juni 28 majira ya saa 3:00 asubuhi katika kitongoji hicho baada ya kumhadaa marehemu na kwenda naye porini ambako yalifanyika mauaji hayo.
Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa George Kyando alisema kuwa marehemu alikuwa akidaiwa mbao mbili na rafiki yake aitwaye Paul Kayuni (50) mkazi wa kitongoji hicho ambazo anadaiwa alimpa rafiki yake huyo.
Baada ya kumdai kwa muda mrefu Pera alikuwa akisumbua kulipa hali iliyomkasilisha mtuhumiwa na kupanga kumpiga kutokana na usumbufu aliokuwa akiufanya.
Siku hiyo mtuhumiwa alimtumia rafiki zake marehemu kuwa waende porini wakamuuzie mbao naye alikubali na alipofika kule polini alimkuta mtu anayemdai ambapo alianza kumshushia kipigo.
Akiwa anampiga marehemu naye aliamua aanze kupigana hali ambayo ilimfanya mtuhumiwa kuchukua panga aliyokuwa ameficha porini na kumkata nayo kichwani ambapo alimsababishia jeraha kubwa lililoanza kuvuja damu nyingi.
Baada ya kuvuja damu nyingi katika jeraha hilo alianguka chini na kupoteza fahamu ambapo walimchukua na kumkimbiza katika zahanati ya kijiji kwaajili ya matibabu.
Alipofikishwa katika zahanati ya kijiji hicho mganga wa zamu alipompokea na kumfanyia uchunguzi aliwaambia amekwisha fariki kutokana na kuvuja damu nyingi kutokana na jeraha alilopata.
Polisi inamshikilia mtuhumiwa wa mauaji hayo na atafikishwa mahakamani pindi upelelezi wa awali utakapokuwa umekamilika.
Mwisho
No comments:
Post a Comment