Thursday, 29 June 2017

Wanawake washauriwa kupata tiba za kitaalamu

Na Gurian Adolf
Sumbawanga. 
Wanaume mkoani Rukwa wametakiwa kuweka kando mifumo kandamizi ya dhidi ya wanawake hivyo waruhusu kwa wake zao wenye kusumbuliwa na maradhi mbalimbali kujitokeza na kupata tiba hospitalini pindi madaktari bingwa watakapowasili mkoani hapa.
Mkazi wa kitongoji cha Jangwani, Pendoeva Kapola alisema hayo jana wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, kuhusu ujio wa madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali wanaoletwa na mfuko wa bima ya afya (NHIF).
Madaktari hao wanaotibu maradhi mbalimbali wanatarajiwa kuwasili na kuanza kutoa tiba mapema juma lijalo katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Rukwa iliyopo mjini Sumbawanga.
Kapola alisema kuwa wapo baadhi ya wanaume wamekuwa wakiendekeza mifumo kandamizi dhidi ya wanawake, kiasi cha kushindwa kuwapata hata ruhusu ya kutoka nyumbani kwao ili waende hospitali kupata tiba hivyo kutibiwa kienyeji hali ambayo imesababisha baadhi ya wanawake kutopata ufumbuzi wa kudumu wa maradhi yao na wakati mwingine kupoteza maisha. 
Alisema mifumo dume na mingine iliyotawala katika jamii inapaswa kuachwa mara moja ili wanawake waweze kujitokeza hospitali na kutumia fursa ya uwepo wa madaktari bingwa kupata tiba ya uhakika ya magonjwa sugu na mengineyo yanayowasumbua.
Aidha, Meneja wa NHIF, Simon Mbaga alisema ujio wa madaktari bingwa ni sehemu ya utekelezaji mpango wa mfuko huo kuyafikia maeneo ya pembezoni ili wagonjwa waweze kupata tiba kutoka kwa wataalamu hao wa afya pasipo kutembea umbali mrefu na kutumia gharama kubwa kuwafuata.
Mbaga alisema kwamba madaktari bingwa watakaokuwepo ni wale wa magonjwa sugu ya ndani pamoja na magonjwa ya moyo, watoto, mfumo wa mkojo, pua, koo, na masikio sambamba na madaktari bingwa wa afya ya uzazi na magonjwa ya wakina mama.
Alisema kwamba wanachama wa Mfuko wa bima ya afya watatibiwa kwa kutumia kadi zao, lakini wale wasio na kadi watalazimika kulipia gharama za kawaida za hospitali.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment