Na Gurian Adolf
Katavi
Wizara ya Maliasili na Utalii imewaonya wafugaji hapa nchini kuacha tabia yakwenda kuchungia mifugo yao katika hifadhi za taifa na mapori ya akiba kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na watambue kuwa hawataepuka mkono wa sheria iwapo watabainika wakiingiza mifugo yao humo.
Amewataka Wahifadhi wote kushirikiana na Mamlaka za Mikoa na Wilaya ili kuweza kukabiliana na tatizo la uvamizi wa maeneo ya hifadhi yanayofanywa kwa ajili ya shughuli za kibinadamu hususani uvamizi wa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi .
Onyo hilo limetolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Generali Gaudence Milanzi alipokua akifunga mafunzo ya uongozi kwa maafisa Wanyama pori yenye lengo la kuwafanya wafanye kazi kutoka mfumo wa kiraia na kuwa mfumo wa kijeshi yaani Jeshi usu, yaliofanyika katika kituo cha mafunzo Mlele Mkoani Katavi .
Alisema kuwa hivi sasa uhifadhi unakabiliwa na tatizo la uvamizi unaonywa kwa shughuli za kibinadamu hususani uchungaji wa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi baadhi ya maeneo hata binadamu kujenga na kuishi ndani ya maeneo ya uhifadhi kitendo ambacho ni kosa kisheria na kamwe hakita vumiliwa.
Meja Jenerali huyo alisema kuwa Wizara inatoa wito kwa Wahifadhi wote na kwa kushirikiana na Mamlaka za Mikoa na Wilaya husika kulimaliza kabisa tatizo hilo.
Aliwaagiza wahitimu wa mafunzo hayo washirikiane na wakuu wao kupanga mipango itakayo washirikisha wananchi katika kumaliza tatizo la uvamizi wa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi na migogoro ya mipaka kati ya maeneo ya hifadhi na Vijiji kwani nalo zimekuwa ni changamoto kubwa.
Milanzi aliwaomba wananchi wote kuendelea kuheshimu sheria za nchi na kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya hifadhi kwani watambue kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Alisema kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni wizara ya Maliasili na Utalii imeshuhudia baadhi ya matukio ya mmomonyoko mkubwa wa maadili hasa kwa watumishi wa kada ya Askari wao wenyewe kujihusisha na vitendo vya ujangili na mengine mambo yasiyo faa katika utumishi wa umma.
Alieleza kuwa mafunzo waliopatiwa wahitimu hao anaamini kuwa kwa kuwa wao ndio viongozi wakuu wa askari watakwenda kusaidia kurudisha nidhamu kwa askari na watumishi wa chini yao kwa kuwaelekeza mambo mazuri ya kujenga wanayotakiwa kuyafanya ili kuhakikisha kunakuwepo na uhifadhi endelevu wa maliasili za nchi.
Kaimu kwaupande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Wanyama pori Tanzania Martin Loibooki alisema ulinzi wa rasilimali za Wanyama pori umeendelea kuimarika ndani na nje ya mapori ya akiba na tengefu sambamba na kuimarisha ukaguzi wa nyara katika maeneo ya mipakani kwa kushirikiana na wadau wengine.
Chini ya uongozi wa Wizara TAWA imeshirikiana na idara ya Wanyama pori ,TANAPA na mamlaka ya hifadhi Ngorongoro NCCA katika kutekeleza kazi mbalimbali.
Mafunzo hayo ya wiki sita yaliwashirikisha wahitimu 97 wakiwemo Maafisa wandamizi 20 na maafisa wa kati 77 wa kutoka Mamlaka ya Wanyama pori Tanzania TAWA.
Mwisho
No comments:
Post a Comment