Friday, 26 May 2017

Washauriwa kutowachukia watoto waliopata mimba

Na Israel  Mwaisaka
Nkasi

JAMII imetakiwa kutowachukia na kuwatenga Watoto wao wa kike pale wanapopata mimba katika umri mdogo na kuachishwa masomo bali wawajengee mazingira mazuri ya kupata elimu nje ya mfumo rasmi na kuweza kutimiza ndoto zao.

Wito huo umetolewa na mkuu wa wilaya Nkasi Said Mtanda kwenye ufunguzi wa mafunzo kwa wadau mbalimbali juu ya mapambano dhidi ya mimba na ndoa za utotoni zilizoandaliwa na shirika lisilo kuwa la kiserikali la KIWOHEDE

Alisema kuwa mimba kwa watoto wa kike zimekuwa zikiwakwaza wazazi wanaowasomesha na mwisho wa siku upata hasira,na kuwa ikifikia hatua hiyo wazazi hawatakiwi kuchukua maamuzi mabaya kwa hasira kwa kuwapiga watoto wao bali kinachotakiwa ni kuanza kutafuta namna nyingine ya kumsaidia mtoto huyo ili aweze kuyafikia malengo yake kwa kupata elimu ya masafa.

Mkuu huyo wa wilaya alidai kuwa wengi wa watoto ujikuta wamepata mimba bila ya wao kutegemea kutokana na umri wao mdogo na kuwa si rahisi kujirudia kufanya kosa hilo kutokana na majuto atakayoyapata na kuwa ni vizuri sasa kuwatengenezea mazingira mazuri watoto hao ya kupata elimu zaidi hata ikiwezekana kuwapatia elimu ya ujuzi wowote ule.

Mratibu wa mafunzo hayo kutoka KIWOHEDE Salimu Mpanda alisema kuwa mafunzo hayo yamewashirikisha watu kutoka katika makundi mbalimbali katika kata ya Chala huku lengo kuu ni kuwajengea uwezo watu namna ya kukabiliana na ndoa za utotoni ambazo zimekua zikiharibu maisha ya watoto wengi wa kike.

Alisema KIWOHEDE katika uchunguzi wao walibaini kuwa eneo la Chala na wilaya nzima ya Nkasi limekuwa likikabiliwa na changamoto hiyo ya Watoto wengi wa kike kupata mimba au kuozwa katika umri mdogo na kuwa ipo haja ya kuanzisha mapambano hayoi katika kukabiliana na hari hiyo.

Naye Diwani wa kata ya Chala Michael Mwanalinze kwa upande wake alilishukuru shirika hilo kwa kuiona changamoto hiyo na kuanzisha mapambano dhidi ya mimba katika umri huo mdogo na kuwataka washiriki wa mafunzo hayo wakaitendee haki elimu watakayoipata hapo kwa kushiriki katika vita hiyo moja kwa moja.

Mwisho

No comments:

Post a Comment