Friday, 26 May 2017

Mtoto auawa kwa kunyongwa na baba wa kambo

Na Gurian  Adolf
Sumbawanga
 
MTOTO Agatha Raphael(2) aliyekuwa akiishi katika kijiji cha Mao wilayani Kalambo mkoani Rukwa amekufa baada ya kunyongwa na baba yake wa kambo. 

Tukio la kunyongwa kwa mtoto huyo lilifanyika Mei 16 majira ya saa 11:00 jioni huko kijiji cha Mao kata ya Mbuluma tarafa ya Matai,wilaya ya Kalambo, mkoa wa Rukwa.

Akitoa  taarifa za tukio hilo Kamanda wa polisi mkoa  wa Rukwa George Kyando alisema kuwa kabla ya mtoto huyo  kuuawa kwa kunyongwa alipotea katika mazingira ya kutatanisha akiwa na baba yake wa kambo.

Alisema kuwa mama mzazi wa mtoto huyo aliyefahamika kwa jina la Anisia Kasiti(22) alikwenda mashineni na kumuacha nyumbani mwanaye huyo.

Kamanda alisema kuwa siku kadhaa kabla mtuhumiwa kufanya mauaji hayo alisikika akiongea kuwa lazima amuue yule mtoto kwani siyo wake.

Baada ya kauli hiyo ambayo ilitishia kuuawa kwa mtoto Agatha ndipo alipotoweka katika Mazingira ya kutatanisha na mnamo Mei 17 mama wa mtoto huyo alienda kutoa taarifa katika uongozi wa kijiji na juhudi za  kumtafuta bila mafanikio.

Siku ya Mei 18 mama wa marehemu alienda kutoa taarifa katika kituo cha polisi matai kuhusu kupotea kwa mwanae Agatha Raphael na jalada la uchunguzi lilifunguliwa ili kumchunguza baba wa kambo kutokana na kauli aliyoitoa hapo awali.

Baada ya taarifa hiyo polisi walimshikilia mtuhumiwa na huku juhudi za kumtafuta mtoto zikiwa zinaendelea.

Kamanda Kyando alisema kuwa siku ya mei 4 majira ya 11:50 jioni mkazi wa kijiji hicho aliyefahamika kwa jina la Aron Mwanambogo, Aligundua kuwepo kwa mwili wa marehemu Agatha shambani kwa mtuhumiwa ukiwa umelala chali kwenye kijito kilichopo ndani ya shamba hilo.

 Baada ya kufanyiwa uchunguzi  wa kitabibu iligundulika kuwa mtoto huyo alikufa kutokana  na kukosa hewa baada ya kunyongwa .

Mtuhumiwa bado anashikiliwa na polisi  na atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi  wa awali kukamilika.
 
Mwili wa marehemu mtoto Agatha umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya kufanya mazishi.

Hata hivyo Kamanda Kyando alitoa wito  kwa wananchi mkoani humo kuacha tabia  ya kujichukulia sheria mikononi na kama kuna  matatizo ya kifamilia na ndoa ni vizuri wanandoa hao wakasuruhishana kupitia kwa viongozi wa ukoo, dini na ikishindikana ni bora kutengana kuliko kufanya mauaji kama ya mtoto Agatha.

Mwisho




No comments:

Post a Comment