Israel Mwaisaka
Nkasi
Mtoto aliyefahamika kwa jina la Florence Kinyonto (2) katika kijiji cha Chala”B”kata ya Chala wilayani Nkasi mkoani Rukwa amekufa maji baada ya kutumbukia kwenye mtaro wa maji machafu maji.
Taarifa zilizopatikana toka kijijini hapo na kuthibitishwa na diwani wa kata hiyo ya Chala Michael Mwanalinze ni kuwa mtoto huyo alifikwa na mauti hayo majira ya saa tano asubuhi alipotumbukia kwenye mfereji wa mto Mkopezi na alikua anamfuata mama yake kwa nyuma aliyekuwa amekwenda dukani kununua karanga za kuunga kwenye mboga.
Mama wa mtoto huyo akiwa hajui kama mtoto huyo alikua akimfuata nyuma ndipo mtoto huyo alijikuta amefika kwenye mfereji wa mto huo na kutumbukia na kupelekea kifo chake baada ya kunywa maji yaliyokuwa katika mfereji huo.
Akitoa ufafanuzi jana Diwani wa kata hiyo Mwanalinze ,juu ya tukio hilo alidai kuwa wakati mama wa mtoto huyo alipokuwa anarudi nyumbani alitupa jicho kwenye mfereji wa mto huo na kuona kiumbe kikielea ndani ya maji na muda mfupi aligundua kiumbe hicho kuwa ni mtoto wake.
Alisema kuwa baada ya tukio hilo ilipigwa mbiu ya kijiji na wakatoa taarifa Polisi ambao walifika kwa haraka katika eneo la tukio na baada ya vipimo na uchunguzi ndugu wa marehemu walikabidhiwa mwili wa marehemu kwa ajiri ya kuendelea na shughuli nyingine za mazishi.
Juhudi za kumpata kamanda wa Polisi mkoani Rukwa George Kyando ili athibitishe tukio hilo ziligonga mwamba baada ya simu yake kuita bila kupokelewa kwa muda mrefu.
Mwisho
No comments:
Post a Comment