Tuesday, 2 May 2017

Mkuu wa mkoa wa Rukwa 'atema cheche'

Israel Mwaisaka
Nkasi

MKUU wa mkoa Rukwa Zelote steven  amewaagiza Waajiri wote mkoani Rukwa  wahakikishe kuwa mabaraza ya Wafanyakazi  yanafanyika kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa ili waweze kupata nafasi ya kujadili mambo yao kwa kina.

Agizo hilo amelitoa jana kwenye sherehe za Mei mosi ambazo kimkoa ziliadhimishwa wilayani Nkasi ambapo alidai kuwa mabaraza ya Wafanyakazi ni muhimu yakafanyika mahali pa kazi kwa uhuru mkubwa na ni jukumu la waajiri kuona mabaraza hayo yanafanyika na kwa kufuata taratibu zilizowekwa.
                                             Mkuu wa mkoa wa Rukwa Zelote Steven

“ufike wakati Waajiri kubadili mawazo juu ya vyama vya Wafanyakazi badala yake wanatakiwa kushirikiana na mabaraza hayo ya wafanyakazi katika kutafuta suluhisho la matatizo kwa wafanyakazi itakayoweza kuleta ufanisi mkubwa mahali pa kazi”alisema zelote

Sambamba na hilo ameziagiza halmashauri zote mkoani Rukwa kuhakikisha kuwa wanayatumia mapato ya ndani katika kujenga nyumba za watumishi wao ili kuweza kupunguza tatizo la uhaba wa nyumba kwa watumishi lililopo kwa sasa.

Alisema moja ya mambo yanayochangia ufanisi mkubwa kwa watumishi ni kuishi kwenye nyumba bora ambazo zitamfanya kuwa huru na kuweza kutekeleza majukumu yao kwa uhuru mkubwa.

Awali ofisa kazi wa mkoa Niseteli Buleti alidai kuwa ofisi yake ndiyo sehemu halisi ya kushughulikia matatizo ya wafanyakazi lakini changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni ya wafanyakazi wengi kushindwa kufika kwenye mashauri pale yanaposikilizwa na kupoteza haki zao za kimsingi.

Hivyo aliwataka wafanyakazi kutokuwa waoga katika kutetea haki zao za msingi na kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa Wafanyakazi  kufika kwenye mashauri pale yanapokuwa yamepelekwa katika ofisi yake ili kuweza kupata haki wanazozistahili.

Sherehe hizo za Meimosi zilikwenda sambamba na kuwazawadia zawadi wafanyakazi bora waliofanya kazi kwa kujituma katika mwaka huu wa 2017
Mwisho

No comments:

Post a Comment