Gurian Adolf
Nkasi
WAUMINI
wa madhehebu ya Kikristu katika kijiji cha Nkana wilayani Nkasi mkoani
Rukwa wameingia katika mgogoro mkubwa kutokana na kugombania eneo la
kuzikia katika kijiji hicho.
Wakristu
hao ambao ni wa makanisa ya Romani Katoliki, Moravian na Assembliss of
God wamejikuta wakivutana vikali kutokana na kugombea eneo la makaburi
ambalo kanisa Katoliki wamekuwa wakidai ni mali yao hivyo waumini wa
makanisa mengine hawapaswi kuzikwa katika makaburi hayo pindi wanapo
fariki dunia.
Akizungumza
na Nipashe mwenyekiti wa kijiji hicho Norbeth Pahali alisema kuwa
mvutano huo umekuwa ni wa muda mrefu sasa ambapo uongozi wa kijiji na
kata umeshindwa kuutatua kutokana na pande hizo kutotaka suluhu.
Alisema
kuwa February 20 aliitisha mkutano wa hadhara kijijini hapo kwa lengo
la kujadili namna ya kutatua mgogoro huo lakini mkutano huo ulivurugika
na kulazimika kuuahirisha kutokana na vuta nikuvute iliyojitokekza kwa
viongozi wa madhehebu hayo katika kijiji hicho.
Pahali
alisema kuwa viongozi wa kanisa Katoliki kijijini hapo wamekuwa wakidai
kuwa hawataki madhehebu mengine wakawazike waumini wao katika makaburi
hayo pindi wanapofariki kwakuwa makaburi hayo ni mali yao kwani kanisa
hilo ndilo kongwe kijijini hapo na lilianzisha makaburi hayo, hivyo
madhehebu mengine nao wakatafute makaburi yao.
Mwenyekiti
huyo wa kijiji cha Nkana alisema kuwa yeye aliwashauri waumini wa
madhehebu nyingine waende mahakamani kwani suala hilo walikwisha
lifikisha ngazi ya kata lakini nayo imeshindwa kutatua mgogoro huo ambao
usipopatiwa ufumbuzi huenda ukapelekea hata uvunjifu wa amani.
Hata
hivyo Gazeti hili liliwasiliana na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya
ya Nkasi Julius Kaondo alisema kuwa ofisi yake haijapokea suala hilo
lakini aliahidi kulifuatilia na kulipatia ufumbuzi haraka iwezekanavyo.
Alisema
kuwa yeye binafsi haoni sababu kwanini kuibuke mvutano huo wakati
madhehebu hayo yote ni ya Kikristu ambayo yanatofautiana tu misingi ya
ibada lakini imani yao ni moja hivyo ni lazima busara itumike ili
kutatua mgogoro huo ambao unaweza kukua iwapo ukifumbiwa macho.
Mkurugenzi
huyo alisema kuwa kazi ya dini ni kusisitiza amani, itakuwa ni ajabu
iwapo viongozi wa madhehebu hayo watashindwa kuafikiana na kusababisha
uvunjifu wa amani kwani ni wajibu wao kuilinda amani na sikuwa chanzo
cha mgawanyiko.
Mwisho
No comments:
Post a Comment