Wednesday, 12 April 2017

Sungusungu Katavi wamuunga mkono Magufuli


Gurian Adolf
Katavi

WALINZI jadi Sungusungu katika Kata ya Mamba Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi wamekabidhi madawati zaidi ya 100 kwa uongozi wa Serikali ya Wilaya ya Mlele yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni tisa kwa ajiri ya kupunguza tatizo la upungufu wa madawati katima shule za Msingi za Halmashauri ya Mpimbwe.

Madawati hayo walikabidhi jana kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Hiyo Elasto Kiwale katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya Mtendaji wa Kata hiyo.

Mwenyekiti wa Sungusungu wa Tarafa ya Mamba Mtamila Mwitasheo alisema katika kumuunga mkono Rais John Magufuli juu ya kuondoa tatizo la upungufu wa madawati katika shule za msingi na sekondari Sungusungu wa Kata ya Mamba wamechangia madawati 105 yenye thamani ya Tshs 9,300,000 kwa ajiri ya shule za Msingi katika Kata hiyo .

Alisema fedha za kutengenezea madawati hayo zilitokana na faini ndogo ndogo ambazo wamekuwa wakiwatoza watu wenye makosa mbalimbali katika kata ndipo Sungusungu waliamua fedha hizo zilizopatikana zitumike kwa ajiri ya kutengeneza madawati .

Mwenyekiti huyo wa Sungusungu alieleza kuwa Watemi wa Sungusungu kwenye shughuli zao za kulinda usalama wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zimeanza kuwakatisha tamaa katika utendaji wao wa kazi za ulinzi .

Katika risala iliyosomwa na Katibu wa Sungusungu wa Kata hiyo Mabula Patrick alieleza kuwa pamoja na kutoa madawati hayo Sungusungu pia wamechangia ujenzi wa vyumba vya madarasa na nyumba za walimu katika Tarafa ya Mamba .

Alisema malengo yao ni kuhakikisha wanamuunga mkono Rais katika kuhakikisha wanamaliza kabisa tatizo la upungufu wa madawati, nyumba za walimu na vyumba vya madarasa.

Kwaupande wake Mkurungezi wa Halmashauri ya Mpimbwe Elasto Kiwale alisema madawati hayo waliokabidhiwa yatasaidia kupunguza tatizo la upungufu wa madawati uliokuwepo katika Halmashauri hiyo .

Aliwaomba pia waendelee kuchangia kwenye sekta nyingine na waendelee kushirikiana na Serikali katika maswala ya kuleta maendeleo kwani Serikali peke yake bila kushirikiana na wananchi haiwezi kutatua changamoto zilizopo.

Pia aliwataka Sungusungu wafanye kazi zao za ulinzi kwenye maeneo yao kwa kuzingatia sheria za nchi ili kuondokana na baadhi ya malalamiko dhidi yao yanayokuwa yanajitokeza wakati wanapofanya shughuli za ulinzi .

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Nyansongo Serengeti alisema pamoja na sungusungu kufanya shughuli za ulinzi wameonyesha mfano wa kuingwa kwa kuchangia maendeleo kwenye jamii.

Alieleza kuwa eneo la Sungusungu ni la muhimu sana kwa kuwa wanalojukumu la kuleta maendeleo kwenye maeneo yao wanayoishi .

Aliwasisitiza wahakikishe wanashirikiana na jeshi la polisi katika kuwafichua na kuwabaini watu wote ambao wanajihusisha na utumiaji na uuzaji wa dawa za kulevya .

Diwani wa Kata ya Mamba Pascal Sanane aliwapongeza Sungusungu hao kwa uzalendo wao wa kuchangia madawati kwani fedha hizo walizozitumia kutengeneza madawati wangewaza kuamua kuzigawana wenyewe lakini hawakufanya hivyo.

Mwisho

No comments:

Post a Comment