Wednesday, 12 April 2017

Hakimu anaswa na rushwa ya 200,000

Gurian Adolf
Nkasi

HAKIMU wa Mahakama ya mwanzo ya Chala wilayani Nkasi mkoani mkoani Rukwa Theobad Buyombo anashikiliwa na taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) wilayani Nkasi kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya Tshs,200,000

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Takukuru  wilayani Nkasi Samson Bishati alisema kuwa hakimu huyo aliomba rushwa kwa Mwananchi mmoja aliyekuwa na shitaka lake la madai katika mahakama hiyo na aliomba apewe kiasi hicho cha fedha ili aweze kupewa upendeleo katika shauri lake hilo.

Alisema kuwa baada ya hapo Takukuru waliweka mtego na kufanikiwa kumkamata hakimu huyo ofisini kwake majira ya saa 11 jioni jana akiwa na fedha hizo zilizotolewa na Takukuru na kufanikiwa kumkamata hakimu huyo.

Amedai kuwa hakimu huyo baada ya kupokea fedha hizo aliziweka kwenye tofali ndani ya ofisi hiyo na kuwa wao wakiwa na viongozi wa kijiji hicho walifanya upekuzi na kuzikuta fedha hizo na kisha kumkamata na kumfikisha Polisi.

Kamanda huyo wa Takukuru amedai kuwa uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo umekamilika na mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa kujibu tuhuma hizo zinazomkabili.
Mwisho

No comments:

Post a Comment