Friday, 21 April 2017

Rukwa wamuomba Magufuli usafiri wa ndege

Gurian  Adolf
Sumbawanga

WANANCHI wa mkoa wa Rukwa wamemuomba rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Maguli kutoa fedha kwajili ya kuukarabati ama kuwajengea uwanja mpya wa kisasa wa ndege ambao unatarajiwa kujengwa katika mji wa Matanga ili nao waweze kunufaika na ndege ambazo amekua akinunua kwaajili ya kutoa huduma kwa wananchi.

Wakizungumza na rukwakwanza.blogspot.com baadhi ya wananchi wa mkoa huo walisema kuwa nao wanahaki kupata ruti ya ndege hizo kwakuwa ni za serikali na zimenunuliwa kwa kodi ya watanzania wakiwamo wakazi hao.

Walisema kuwa ndege hizo zinaishia katika mkoa wa Mbeya lakini mkoa wa Rukwa hakuna ruti hivyo wakitaka kusafiri kwa kutumia ndege wanalazimika kusafiri kwa basi hadi mkoani Songwe ndipo wakapande ndege kuelekea jijini Dar es salaam.

Mmoja wa wananchi hao Fransis Sebastian alisema kuwa moja kati ya changamoto kubwa iliyopo ni mkoa wa Rukwa ni kukosa uwanja wa kisasa hivyo wanamuomba rais aweze kutoa fedha ili kujenga uwanja wa ndege ama kuuboresha uliopo walau na wakazi wa mkoa wa Rukwa waanze kusafiri kwa njia ya anga.

Alisema kuwa inawachukua siku mbili kutoka Sumbawanga mpaka jijini Dar es salaam lakini kungekuwa na usafiri wa ndege ingekua ni rahisi kwani wangekuwa wanakwenda na kufanya shughuli kisha kurejea mkoani humo kwakua kunausafiri wa ndege.

Naye Flora Mwaga mkazi wa mji wa Sumbawanga alisema kuwa watajiona fahari kusafiri kwa ndege za serikali kwani wataziwezesha kupata kipato haraka na kununua ndege nyingine kwakuwa watakuwa wanasafiri na ndege za serikali.

Alisema kuwa yapo baadhi ya  mashirika ya ndege za ya watu binafsi ambayo hufanya safari mara moja moja mkoani humo lakini wamekuwa wakiwalangua kwa bei kubwa na safari zake hazina uhakika ila anaamini kuwa bei ya ndege za serikali itakuwa siyo ya kulangua kwakua itazingatia kipato cha mkulima wa mkoa wa Rukwa.

Alisema kuwa bado baadhi ya watu wanaona kama kusafiri kwa ndege ni ajabu ama anasa lakini hiyo ni kutokana na bei wanayolanguliwa na wafanyabishara ya usafiri wa anga binafsi ila anauhakika kama bei itazingaitia maisha ya kitanzania watamudu kupanda ndege hizo kwakuwa hazitumii gharama kubwa kuziendesha na zitawarahisishia kusafiri na kufanya mambo yao kwa wakati.

Alisema kuwa rais anapaswa kutupia jicho la pekee kwa mikoa ambayo kwa miaka mingi imekuwa haina usafiri wa anga ili nayo ifunguke kwakua pia kuna fursa za kitalii katika mikoa hiyo lakini watalii wanashindwa kuifikia kutokana na kutokuwepo na usafiri wa anga ambao unachukua muda mfupi na nisalama.

Akitolea mfano vivutio hivyo alisema ni kuwepo kwa maporomoko ya kalambo falls, mapori ya akiba, hifadhi ya taifa ya Katavi, ziwa Rukwa, ziwa Tanganyika, meli kongwe duniani ya mv Liemba, Kasanga Bismark port ambayo ni kivutio kikubwa kwa Wajerumani, msitu wa mbizi na vingine vingi ambavyo ni fursa ya utalii ambavyo vingeliingizia taifa na mkoa huo fedha nyingi za kigeni licha ya kuwa bado havijatangazwa na kujulikana ambavyo vinaweza vutia watalii.

Alisema kuwa mkoa wa Rukwa umejaliwa kuwa na mbega wekundu, samaki wa mapambo, mlima itwelele alama za nyayo za binadamu juu ya mawe, bao likiwa limechongwa kwenye jiwe, chemchemi ya za maji ya moto na mengineyo mengi ambayo hayajulikani na nifursa lakini yamebaki kuwa mambo ya kawaida tu kwakuwa hayajulikani na hakuna anae yasemea na pia kuwepo kwa changamoto ya usafiri kwa njia ya anga.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment