Saturday, 15 April 2017

Mtoto afariki dunia baada ya kuumwa na nyuki

Gurian  Adolf
Nkasi
 
MTOTO mmoja wilayani Nkasi mkoani Rukwa amefariki dunia baada ya kuumwa na nyuk wakati akichunga ng'ombe za familia yao.
Katika tukio la kwanza lililotokea katika kijiji cha Kisura kata ya Nkandasi wilayani Nkasi mtoto aliyefahamika kwa jina la Debora Mata(4) alifariki dunia muda mfupi baada ya kushambuliwa na nyuki.
Akizungumzia tukio hilo Mwenyekti wa kijiji hicho Focus Mwanandenje alisema kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 14 majira ya saa 12;30 za jioni wakati watoto wa familia moja Debora na Aneth(7) wakiwa wanatoka kuchunga ng'ombe za nyumbani kwao.
Alisema kuwa wakiwa njiani wanarejea kutoka huko porini mmoja kati ya ng'ombe waliokuwa wakiwachunga alikwenda kuugonga mti ambao  kulikuwa na lundo la nyuki kitendo kilichosababisha lundo hilo la nyuki kuanguka chini.
Baada ya nyuki hao kuanza kuruka walianza kuwashambulia watoto hao katika sehemu mbalimbali za miili yao kwakuwa Debora alikuwa ni mdogo alishindwa kukimbia na nyuki walimuuma mpaka akazidiwa.
Aneth yeye kwakua alikuwa ni mkubwa alifanikiwa kukimbia licha ya kuwa naye alikuwa ameumwa na nyuki hao ambapo aliweza kutoa taarifa kijijini juu ya tukio hilo lililowapata.
Baada ya wakazi wa kijiji hicho kwenda eneo la tukio walimkuta mtoto Debora akiwa ameumwa na hari yake ni mbaya ambapo walimpeleka katika zahanati ya kijiji hicho lakini alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa katika zahanati hiyo.
Mwenyekiti Mwanandenje alisema kuwa Aneth aliweza kupatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri licha ya kuwa bado amevimba kutokana na kuumwa na nyuki katika mwili wake.
Kwaupande wake baba wa watoto hao Deus Matema alisema kuwa ameupokea kwa masikitiko msiba wa mtoto huyo lakini hana la kufanya kwakuwa imetokea na anaamini ni mapenzi ya Mungu.

No comments:

Post a Comment