Israel Mwaisaka,
Nkasi
WANANCHI wa kijiji cha Londokazi kata ya Chala wilayani Nkasi mkoani Rukwa jana walijikuta katika taharuki baada ya Mwanamke mmoja kijijini hapo aliyefahamika kwa jina la Jenimary Wambari (20) kudaiwa kujifungua mtoto na kumtupia chooni.
Baada ya taarifa hizo kuzagaa kijijini humo wakazi wa kijiji hicho walikusanyika nyumbani kwao na Mwanamke huyo na kuwa na sintofahamu ya nini cha kufanya baada ya kutokea kwa tukio hilo.
Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi mwenyekiti wa kijiji hicho Parasido Andara alisema kuwa baada ya mazingira hayo aliamua kutoa taarifa Polisi ambapo waliweza kufika haraka katika eneo la tukio na walishirikiana na wakazi wa kijiji hicho kuanza kukibomoa choo hicho kwa lengo la kukitoa kichanga hicho kilichotumbukizwa ndani ya choo.
Alisema baada ya zoezi hilo kufanyika jitihada za kumpata mtoto huyo akiwa hai ziligonga mwamba baada ya choo hicho kilichojengwa kienyeji kuwa na maji mengi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwa sasa.
Mwanamke huyo baada ya kuhojiwa akiwa ametapakaa damu nyingi mwilini alisema kuwa yeye hatambui nini kimemtokea na ndipo walipomchukua na kumpeleka katika kituo cha afya cha Chala na kubaini kuwa alikua na ujauzito wa miezi mitano ambao hakuwa nao tena kwa wakati huo.
Akijitetea katika mahojiano katika kituo cha polisi Mwanamke huyo akikiri kuwa na ujauzito wa miezi mitano lakini alibanwa na haja na baada ya kufika chooni alishangaa kuona mtoto huyo akitumbukia chooni bila ya yeye kujua.
Diwani wa kata hiyo Michael Mwanalinze amekiri kutokea kwa tukio hilo na kuwa Mwanamke huyo bado anashikiliwa na jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi.
mwisho
No comments:
Post a Comment