Wednesday, 19 April 2017

Manispaa ya Sumbawanga wamaliza siku tatu bila kula nyama

Gurian  Adolf
Sumbawanga
 
WAKAZI wa mji wa Sumbawanga mkoani Rukwa leo wametimiza siku tatu bila kula kitoweo cha nyama ya ng'ombe,mbuzi na kondoo baada ya wafanyabiashara hiyo kugoma wakiishinikiza serikali iwaruhusu kupitisha ng'ombe walio nunua kwa wafugaji katika barabara ya lami.

Wafanyabiashara hao wamekuwa wakilalamikia kitendo cha kukamatwa na polisi na kutozwa faini ya sh 1,000,000 wakidai kuwa adhabu hiyo inawasababishia hasara.

Wakizungumza katika kikao maalumu ambacho kiliwakutanisha wafanyabishara hao na mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Dkt Halfan Haule ambacho kilikuwa na lengo la kumaliza mgomo huo walidai kuwa wameamua kugoma kwakuwa serikali inawazuia kupitisha ng'ombe katika barabara za lami.

Katika kikao hicho wafanyabiashara hao walilalamikia kitendo cha kutozwa faini ya sh 1,000,000 pindi wanapokamatwa wanapitisha ng'ombe kwa kuwaswaga katika barabara ya lami kwa madai kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria na wanaharibu barabara hizo.

Mmoja wa wafanyabishara hao Dckson Mchunguzi alisema kuwa wao wamekuwa wakipitisha ng'ombe katika barabara ya lami kwakuwa hawawezi kupita pembeni kwani kuna mashamba na iwapo ng'ombe hao wakila mahindi ya wakulima unaibuka mgogoro baina yao na wakulima.

Alisema kuwa baadhi yao wanamitaji midogo hivyo hawana uwezo wa kukodi magari ya kubebea ng'ombe ndiyo maana wamekuwa wakiwasafirisha kwa kuwaswaga kwa kupita kwenye barabara za lami.

Muchunguzi alisema kuwa  wameshindwa kuchinja ng'ombe kwa takribani siku tatu sasa kwakuwa wananshindwa kuwasafirisha ng'ombe hao kutokana na kuzuiwa kuwapitisha kwenye lami.

Naye Samweli Kisabwiti alisema kuwa pia halmashauri ya manispaa imekuwa ikiwatoza ushuru mkubwa wa shilingi 6,000 kila ng'ombe anaechinjwa fedha ambazo ni nyingi tofauti na mikoa mingine ambayo wanatozwa shilingi 2,500.

Alisema kuwa pamoja na kutozwa ushuru huo lakini bado miundo mbinu ni mibovu katika machinjio ya Sumbawanga mjini hali ambayo wanaona hakuna tija inayopatikana kutokana na ushuru wanaotoa.

Akijibu malalamiko yako mkuu huyo wa wilaya ya Sumbawanga alisema kuwa kamwe serikali ya wilaya haipo tayari kukiuka sheria na kuwaruhusu wapitishe mifugo katika barabara ya lami kwakuwa sio tu kuwa ni kosa kisheria bali pia ni uharibifu wa barabara hizo.

Alisema kuwa faini wanazotozwa ni sahihi kwani ndivyo sheria inavyoelekeza na pia inaelekeza kifungo cha miaka mitatu ama vyote pamoja kwahiyo nivizuri kuheshimu sheria.

Mkuu wa wilaya Dkt Haule alisema kuwa kitendo cha wafanyabiashara kugoma wamekiuka masharti ya leseni hivyo faini yake wanapaswa kulipa sh 250,000 na kwa yeyote ambaye hakubaliani na sheria ni bora akabadili biashara lakini kamwe yeye hatatoa maelekezo yanayopingana na sheria.

Alisema kuwa haiwezekani kila mtu ama kundi likajiamlia mambo yake bila kufuata sheria kwani itakuwa ni vurugu hivyo wanapashwa kuheshimu sheria ambayo hairuhusu kupitisha mifugo barabarani.

Aidha alitoa wito wa wafugaji hao kuwa wepesi wa kuziona mamlaka kupitia umoja wao pindi kunapojitokeza sintofahamu kuliko kukimbilia kugoma kwani watendaji wa serikali wapo tayari kuwahudumia lakini kwa kufuata sheria za nchi na si kufuata utashi wa mtu ama kundi la watu.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment