KUTOKANA na kuchelewa kutolewa kwa maamuzi kwa baadhi ya watendaji wa idara ya afya mkoani Rukwa kumeelezwa kuwa kunachangia kuongezeka kwa vifo vya wanawake wajawazito mkoani humo.Imeelezwa.
Hayo yameelezwa na muuguzi mkuu wa wardi ya wazazi ya hospitali ya mkoa wa Rukwa Fides Mayoka wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi aliyetaka kujua ni vikwazo gani wanavyokabiliana navyo katika jitihada za kupambana na ongezeko la vifo vya wanawake wajawazito mkoani humo.
Alisema kuwa miongoni mwa sababu kubwa zinazo changia vifo vya wanawake wajawazito ni kuchelewa kutolewa maamuzi na wahudmu wa afya wa maeneo ya vijijini kwani wanachukua muda mrefu kukaa na mama mjamzito wakati hawana uwezo wa kumsaidia kutokana na huduma inayohitajika.
Mayoka alisema kuwa utakuta mama mjamzito amefikia katika kiwango cha kufanyiwa upasuaji lakini wahudumu hao bado hawafanyi maamuzi ya haraka ya kumruhusu mama huyo afikishwe katika kituo kinachotoa huduma za upasuaji kwa wakati.
Alisema baadhi ya wanawake wajawazito wanafikishwa katika vituo vinavyotoa huduma za uppasuaji wakiwa katika hali mbaya kitendo kinachosababisha kushindwa kuokoa maisha ya mama na mtoto kutokana na kile kinacho onekana kama ni uzembe wa wahudumu wa afya.
Muuguzi huyo alisema kuwa tatizo jingine ni hospitali ya mkoa wa Rukwa ambayo pia ni hospitali ya rufaa kwa mikoa ya Rukwa na Katavi ni kukosa daktari bingwa wa upasuaji kutokana na aliyekuwepo kustaafu hali ambayo imesababisha baadhi ya wanawake wajawazito wenye matatizo makubwa kutopatiwa huduma hiyo kwa wakati.
Alisema kuwa daktari aliyekuwepo alikuwa peke yake akifanya shughuli hiyo ambapo amedumu katika hospitali hiyo kwa miaka 18 na tangu alipo staafu hakuna daktari mwingine aliyepatikana na hivyo kuwepo na pengo kwani mtaalamu wa aina hiyo anahitajika ili kukabiliana na vifo vya wakina mama wajawazito mkoani humo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment