Wednesday, 18 December 2013

AJALI YAUA MMOJA 19 WAJERUHIWA KATAVI



MKAZI wa Kijiji  cha Mwese  Wilaya ya Mpanda, Beritine Bartazal (42) amefariki dunia baada ya  basi dogo alilokuwa akisafiria kuacha njia na kupinduka na kusababisha watu wengine  19 kupata majeruhi na  kulazwa  Hospitali ya wilaya mjini Mpanda.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa  Katavi, Dhahiri Kidavashari  alisema kuwa ajali hiyo ilihusisha basi dogo aina ya Hino lenye namba za usajili  T 894 APW  lililokuwa likiendeshwa  na mmiiliki wa gari hilo Dickson  Kinyonto ambaye alitoroka baada ya kutokea tukio.

Kidavashari  alisema kuwa ajali hiyo ilitokea hapo Desemba 16 saa 6:30 mchana katika eneo la Ilembo  umbali wa kilimeta tatu kutoka Mpanda mjini  barabara  ya Mpanda ya kwenda  Sumbawanga  Mkoa wa Rukwa.

Alisema gari hilo ambalo lilikuwa litikokea  Tarafa ya Mpimbwe Wilaya ya Mlele  likielekea Mpanda  mjini lilipata ajali hiyo baada ya tairi la mbele la upande wa kushoto kupasuka  na ndipo lilipoacha njia  na kupinduka na kusababisha kifo cha  Bartazal na majeruhi 19 ambao wamelazwa katika Hospitali ya wilaya ya Mpanda na watatu kati yao hali zao zikielezwa ni mbaya.

Kwa mujibu wa kamanda Kidavashari, Polisi inaendelea  kumsaka mtuhumiwa Kinyonto  ambaye alitoroka  baada ya tukio ili aweze kufukishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

No comments:

Post a Comment