Na Walter Mguluchuma
Katavi
Mfuko wa hifadhi ya Jamii TASAF katika Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi umefanikiwa kuzilipa kaya masikini zaidi ya shilingi milioni 67 imeanzisha utaratibu mpya kwa njia ya mtandao sambamba na kuwafungulia akaunti Benki bure.
Afisa ufuatiliaji wa TASAF katika Manispaa ya Mpanda Twambulile Solomon alisema hayo hivi karibuni ambapo alisema kuwa utaratibu huo mpya kwa walengwa wa mfuko huo ulianza mwezi julai mwaka jana katika Manispaa hiyo.
Alisema kuwa mpaka sasa utaratibu huo hapa nchini umefanyika katika halmashauri 16 kwa ajiri ya majaribio na kwa mkoa wa Katavi unafanyika katika Manispaa ya Mpanda huku lengo likiwa ni kutaka malipo kwa njia ya mtandao yafanyike katika h almashauri zote za Mkoa wa Katavi kwa njia hiyo .
Twambulile alisema kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka jana hadi sasa wamelipa walengwa malipo yao kwa njia ya mtandao kiasi cha shilingi milioni 67,459,500.
Alifafanua kuwa hadi kufikia mwezi wa pili mwaka huu dirisha lilikuwa linawalipa walengwa 344 kwa njia ya mtandao ambapo kwa kipindi cha mwezi Machi na April walengwa wengine 300 wamejiunga na utaratibu huo wa kulipwa kwa njia ya mtandao.
Afisa ufuatiliaji huyo wa Tasaf alisema kwa kipindi cha mwezi Aprili wameweza kuwafungulia walengwa 71 akaunti katika Benki ya CRDB Tawi la Mpanda bila malipo yoyote na akaunti zao hazitakuwa na makato yoyote.
Aliitaja mitaa ambayo walengwa wamefunguliwa akauti Benki kuwa ni Kawajense walengwa 30 Kamakuka walengwa 14, Mbugani Kakese walengwa walengwa 24 na Kijiji cha Mwamkulu walengwa 4.
Mmoja wa walengwa hao Salome John alisema kuwa utaratibu huo utawazidi kuwahakikishia usalama wa fedha zao kuliko ilivyokuwa awali na utawapunguzia usumbufu wa kupanga foleni kwenye malipo.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kawajense Simon Jumapili alisema utaratibu huo wa malipo kwa njia ya mtandao utawasaidia walengwa kwenda kuchukua fedha zao kwa muda wanaotaka wao tofauti na hapo awali walipokuwa wakipangiwa muda wa kwenda kuchukua fedha.
Pia alisema utawafanya walengwa wa mfuko kwenda kuchukua fedha zao pindi wanapokuwa wamemaliza shughuli zao za nyumbani na hivyo kuto athiri muda wa uzalishaji mali.
Mwisho
No comments:
Post a Comment