Thursday, 8 March 2018

ukiukwaji sheria ya manunuzi, kikwazo miradi ya maji

Na Gurian Adolf
Sumbawanga

IMEBAINIKA kuwa miradi mingi ya maji imekuwa ikitekelezwa chini ya kiwango kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya kutozingatia sheria ya manunuzi(PPRA) na hivyo kuisababishia serikali hasara.
Hayo yalibainishwa jana na waziri wa maji na umwagiliaji mhandisi Isac Kamwelwe wakati akikagua mradi wa maji uliopo katika mji mdogo wa Laela wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa alipokuwa katika ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Alisema kuwa wahandisi wasimamizi wa serikali ambao wanasimamia miradi hiyo na kusaini mikataba kwaniaba ya serikali wamekuwa wakikiuka baadhi ya vipengele katika sheria ya manunuzi kitendo kinachochangia kuisababishia hasara serikali.
Mhandisi Kamwelwe alisema kuwa kwamfano sheria ya manunuzi inataka mkandarasi kulipwa asilimia 15 lakini wao wamekuwa wakilipa mpaka asilimia 20 kitu ambacho ni makosa na ukiukwaji mkubwa wa sheria hiyo.
Alisema kuwa baadhi ya wahandisi wa serikali hawana hata vitabu vya sheria ya manununuzi na hivyo kufanya kazi bila kufuata taratibu hali ambayo lazima wabadirike kama kweli wanania ya kuisaidia serikali.
Pia Waziri huyo alisema kuwa changamoto nyingine kubwa iliyopo ni kuwa hapa nchini hakuna tasisi inayoshughurika na kukagua ubora wa teknolojia kitendo kinachosababisha serikali kuuziwa vitu vilivyo chini ya kiwango ama kupitwa na wakati.
Alisema kuwa miradi mingi ya maji imefungwa panel za solar kwaajili ya kuzalisha umeme wa nguvu za jua kwaajili ya kusukuma pampu za mashine ya maji lakini hakuna tasisi inayopima ubora wa teknolojia iliyotumika kutengeneza solar hizo na hivyo matokeo yake serikali imekuwa ikiuziwa solar bandia ambazo zinashindwa kufanya kazi na hivyo kupata hasara.
Kamwelwe alisema kuwa miradi mingi ya maji imekuwa na changamoto ya nishati ya umeme na hivyo kushindwa kutoa maji kwani solar nyingi hazina uwezo wa kuzalisha umeme pindi mwanga wa jua unapo pungua na hivyo lengo la serikali kuwapa maji wananchi linakuwa halijafikiwa.
Alisema kutoka na hali hiyo ameziagiza tasisi za CRB pamona na ERB kupitia katika miradi ya maji mkoani Rukwa ili iweze kukagua na kubaini mapungufu kisha kutoa mapendekezo nini kifanyike ili wananchi waweze kupata maji.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Kwela wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa Ignas Malocha alimuomba waziri huyo kuiongezea fedha za miradi halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga kwani bado kunachangamoto kubwa ya uhaba wa maji.
Naye mbunge wa jimbo la Sumbawanga mjini Aesh Hillary alimuomba waziri huyo kuiruhusu mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira SUWASA kuanza kupeleka miundombinu ya maji katika eneo la Katumba ambalo limepimwa viwanja vipya zaidi ya 2000 ambapo unatarajiwa kujengwa mji wa kisasa katika Manispaa ya Sumbawanga.
Mwisho

No comments:

Post a Comment