Tuesday, 13 March 2018

Serikali kuanzisha mpango wa kulipia kidogo kidogo bima ya afya

Na Gurian Adolf
Sumbawanga

SERIKALI imesema ina andaa mpango kwaajili ya wananchi kulipia fedha kidogo kidogo  ili kwa atakaye kamilisha atapata fursa ya kujiunga na mfuko wa bima ya afya (NHIF) wa Taifa.

Waziri wa afya,maendeleo ya jamii,jinsia na watoto Ummy Mwalimu aliyasema hayo hivi karibuni mjini Sumbawanga wakati akikabidhi mabati 100 kwaajili ya ujenzi wa kituo cha afya Tambaruka kilichopo wilayani Nkasi yaliyotolewa na mfuko wa bima ya afya NHIF mkoani Rukwa.
Alisema kuwa serikali imebaini wananchi wengi wanashindwa kulipia gharama ya matibabu ya kwa mara moja hali ambayo serikali inaandaa mpango ili wananchi walipie kiasi kidogo kidogo atakapo kamilisha kiwango kinachitakiwa anapewa kadi ya uanachama ya mfuko wa NHIF ambapo atapata fursa ya matibabu.
Waziri huyo wa afya alisema kuwa kwa mtu ambaye si mtumishi wa umma anapaswa kulipia shilingi milioni 1.5 ili ajiunge na mfuko huo fedha ambazo ni nyingi kwani baadhi ya wananchi hususani wa vijijini wamekuwa wakishindwa na hivyo kukosa fursa ya kuwa wanachama wa NHIF na kupata haki ya kutibiwa katika vituo zaidi ya 7,000 ambazo vinatoa huduma za bima ya afya nchi nzima.
Hata hivyo waziri Ummy aliwasisitiza wananchi wa mkoa huo kujiunga na mfuko wa afya ya jamii CHF ambayo inagharimu kiasi cha shilingi 10,000 ambapo watapata fursa ya matibabu kwa watu watano katika kaya na kujihakikishia matibabu katika maeneo yao kuliko kukosa kabisa huduma za afya kwakuwa magonjwa huwafika binadamu bila taarifa na wakati mwingine wanakuwa katika hali mbaya ya kiuchumi.
Naye meneja wa bima ya afya mkoani Rukwa Simon Mbaga aliwasihi wazazi kuwalipia watoto wao shilingi 50,400 ambapo watasajiliwa na huduma za Toto  Afya kadi ambapo watapata fursa ya kutibiwa katika vituo vinavyotoa huduma za bima ya afya ya Taifa ndani na nje ya mkoa huo.
Kwaupande Mbunge wa jimbo la Nkasi Kaskazini Ally Kessy aliushukuru mfuko huo wa bima ya afya kwa kutoa mabati hayo ambapo alisema kuwa yatasaidia katika ujenzi wa kituo cha afya cha Tambaruka.
Pia mbunge huyo alimuomba waziri wa afya kuona namna ya kuusaidia mkoa wa Rukwa ili uweze kujenga vituo vya kutosha vya afya kwani unakabiliwa na uhaba mkubwa na hivyo kushindwa kutekeleza ilani ya chama cha mapinduzi inayotaka kila kata kuwa na kituo cha afya.
Mwisho

No comments:

Post a Comment