Na Gurian Adolf
Kalambo
MWANAMKE aliyefahamika
kwa jina la Maria Sekaye(60) mkazi wa kijijii cha Ilambila wilayani Kalambo ameuawa baada ya kukanyagwa na tembo waliokuwa
njiani wakitokea katika pori la akiba la Lwafu mkoani Rukwa kuelekea katika
nchi jirani ya Zambia.
Akizungumzia tukio hilo diwani wa kata ya Mkowe Alfred Mpandasharo
alisema kuwa tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 4 za asubuhi wakati
mwanamke huyo akiwa ametoka kutembelea shamba lake lililokuwa limevamiwa na
mazao kuliwa na tembo hao.
Alisema kuwa Maria akiwa njiani kurejea kijijini ghafla
alikutana na kundi kubwa la tembo waliokuwa na hasira wakiwa wamechokozwa na
vijana wa kijiji hicho kutokana na kuwafukuza kwa makelele ili waondoke
kijijini hapo waache kula mazao katika mashamba yao.
Diwani huyo alisema kuwa baada ya kundi hilo la tembo kumkuta mwanamke huyo
lilimvamia na kuanguka chini ambapo alikanyagwa na kufa papo hapo.
Naye mkuu wa wilaya ya Kalambo Julieth Binyura aliwaonya
wananchi wanao wafukuza hovyo tembo hao waache tabia hiyo kwani ni hatari kwa
usalama wao wasubiri watendaji wa maliasili ambao watafika kwaajili ya
kuwafukuza kijijini hapo.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa kwa kawaida katika vijiji vya Sundu,Mkowe Ilambila na Katete huwa ni mapito
ya tembo ambapo mara kwa mara wamekuwa wakipita kuelekea nchini Zambia na
baadaye kurejea tena nchini katika pori la akiba la Lwafu.
Alisema kuwa nivizuri wananchi wakaacha kufanya kilimo na
kujenga makazi katika mapito ya tembo hao kwakuwa kawaida huwa hawaachi kupita
hata kama itachukua miaka mingi lakini kunasiku watarejea na kupita tena hivyo
ni hatari kwao.
Mwisho
No comments:
Post a Comment