Saturday, 16 December 2017

IGP awaomba viongozi wa dini

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
JESHI la polisi nchini limewaomba viongozi wa dini mkoani Rukwa Kuongeza bidii katika kuhubiri amani ili mauaji yanayotokana na imani za kishirikina na mapenzi yapungue mkoani humo. 

Mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP, Simon Siro aliyasema hayo jana wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua mikakati ya jeshi hilo katika kukabiliana na mauaji mkoani humo.

Alisema kuwa jeshi la polisi linajitahidi kukabiliana na mauaji yote yanayotokea nchini lakini katika Mkoa wa Rukwa takwimu zinaonesha kuwa mauaji yanayotokana na ushirikina pamoja na  wivu wa mapenzi yanaongoza mkoani humo.

Kamanda Siro alisema kuwa viongozi wa dini wanajukumu kubwa katika kuhakikisha wanahubiri amani ili mauaji hayo yaweze kupungua kwani juhudi hizo zinapaswa kuwa za pamoja kwakua nao wananafasi kubwa la kuwalea wananchi kiroho.

"napenda kuwaomba viongozi wa dini wahusike kikamilifu katika vita ya kumaliza mauaji yanayotokana na imani za kishirikina na wivu wa kimapenzi, na wananchi kabla ya kufanya vitendo hivyo nilazima watafakari kwani mtu ukiua unahukumiwa kunyongwa,unawaacha watoto wako yatima na kuwaharibia maisha kwani watakosa malezi ya wazazi"

Aidha kamanda IGP aliahidi kuwa Jeshi hilo kupitia bajeti zake kuwa litajenga kituo kipya cha polisi cha Sumbawanga mjini kwa kuwa kilichopo ni kichakavu na majengo yanayotumika yalirithiwa kutoka kwa wakoloni.

Pia ameahidi kuupatia mkoa wa Rukwa gari moja jipya aina ya Lori litakalo saidia kutumika katika matumizi mbalimbali ya polisi mkoani humo kwakua kuna upungufu wa vitendea kazi. 

Hata hivyo amewataka wananchi mkoani humo Kushirikiana na jeshi la polisi na kubadirika kuacha kubweteka kwani hivi sasa maisha yamekuwa tofauti na matukio mbalimbali yamekuwa yakiongezeka ni jukumu lao kujijali na kujiepusha kutofanya uhalifu. 

Naye Mwenyekiti wa ulinzi na usalama Wa mkoa wa Rukwa,ambaye ni mkuu wa mkoa huo Joachim Wangabo alimwambia IGP kuwa atajitahidi kuwashirikisha wafanyabiashara mkoani humo ili waweze kujenga nyumba za kuishi polisi kwakua hawawezi kusubiri mpaka serikali ifanye kazi hiyo. 

Mwisho
 

No comments:

Post a Comment