Sunday, 12 November 2017

Walimu watakiwa kutimiza wajibu

Na Gurian Adolf
Kalambo
CHAMA cha walimu CWT wilayani Kalambo mkoani Rukwa kimewataka walimu kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kabla ya kudai haki mbalimbali ikiwemo nyongeza ya mshahara.

Ushauri huo umetolewa jana na katibu wa chama hicho Peter Simwanza wakati wa sherehe maalumu za kuwapongeza walimu wa shule za msingi zilizopo katika kata ya Ulumi ambao wanafunzi wao walifaulu vizuri na kupata kiwango cha alama A katika masomo ya kuhitimu darasa la saba pamoja na shule zilizofanya vizuri.

Alisema kuwa baadhi ya walimu wamekuwa mbele katika kudai haki zao mbalimbali ikiwemo nyongeza ya mshahara lakini hawatimizi wajibu wao kwamujibu wa sheria. 

Katibu huyo alisema kuwa wapo walimu ambao hawawajibiki ipasavyo katika ajira zao lakini ndio vinara katika kulalamikia nyongeza za mishahara na marupurupu mengine lakini kitendo ambacho si sawa kwani haki inaendena na wajibu.

Simwanza alisema kuwa walimu wilayani humo wanapaswa kutekeleza sheria zote za kazi kwa mujibu wa mkataba wa ajira ndipo wadai haki zao kwa mwajiri. 

Aliwataka walimu hao kutokuwa wanyonge pindi wanapoona haki zao zimekiukwa kwani wanapaswa kutambua maslahi yao yapo mikononi mwao lakini kwa kufuata sheria,kanuni na taratibu. 

Aliwaonya walimu hao kuepuka mihemko ya kisiasa katika maeneo ya kazi kwani imekuwa ikisababisha migogoro baina yao na waajiri kwani wamekuwa wakidai haki zao kwa jazba na wakati mwingine kufanya siasa sehemu za kazi sambamba na kuvaa sare za vya katika maeneo ya kazi. 

Naye Sabina Mwamwezi mwakilishi wa walimu kitengo cha wanawake katika chama hicho aliwasihi walimu wa kike wilayani humo kuhakikisha wanajali haiba katika suala la mavazi ili kulinda maadili ya wanafunzi. 

Aliwakumbusha walimu wa kike kuhakikisha kuwa wanakuwa ni mfano wa kuigwa kwa mavazi,kauli kwani wananchi wengi hasa maeneo ya vijijini wamekuwa wakiwatazama kama kioo hivyo ni lazima waiheshimu hadhi wanayopewa na jamii. 

Kwaupande wake mwalimu Zainab Omary wa shule ya msingi Ulumi ambaye wanafunzi walipata alama A wengi katika somo analofundisha la kiswahili alisema kuwa mafanikio makubwa yalitokana na yeye binafsi kulipenda somo hilo sambamba na kujituma katika kufundisha pia kuwapenda wanafunzi wake. 

Mwisho

No comments:

Post a Comment