Na Gurian Adolf
Nkasi
JUMLA ya ng'ombe kumi wamekufa baada ya kupigwa radi wakati wakiwa machungoni huku mchunga ng'ombe hao Ahmad Katunzi (15) akinusurika kifo.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Rukwa , George Kyando amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea juzi majira ya saa 11 jioni katika kijiji cha China kilichopo Kata ya Kate wilayani Nkasi .
Akisimulia mkasa huo mwenyekiti wa kijiji hicho , Joseph Ndasi ambaye pia ndiye mwenye mifugo hiyo alisema jioni ya tukio hilo Ahmad alikuwa akichunga ng’ombe wapatao 22 ambapo ghafla radi ilipiga na kuua ng’ombe kumi papo hapo .
“Katika tukio hilo mchungaji Ahamd alijikuta kimerushwa mita kumi hivi kutoka alipokuwa amesimama ambapo amepata majeraha madogo madogo … ngombe wengine kumi na mbili wamenusurika ila kwa hofu wote walikimbia na kurejea nyumbani “ alisema.
Hata hivyo kamanda wa polisi mkoani humo aliwasihi wachungaji kurejea nyumbani mara moja pindi wanapoona dalili za mvua kwani ni hatari kwa maisha yao na wanyama hao.
Taarifa kutoka kijijini zinakumbusha usemi wa wahenga usemao kufa kufaana kwani wakazi kijiji hicho walivamia mizoga ya wanayama hao na kuanza kuagawana nyama kwaajili ya kitoweo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment