Na Israel Mwaisaka
Nkasi
KUTOKANA na matokea mabaya ya mitihani ya taifa kwa shule za sekondari wilayani Nkasi idara ya elimu mkoani Rukwa imeitisha kikao cha Tathimini na kushirikisha wadau mbalimbali ili kuweza kubaini tatizo linalopelekea wilaya Nkasi kushindwa kufanya vizuri katika mitihani ya kidato cha Nne.
Akifungua kikao hicho cha Tahmini katibu tawala wa wilaya Nkasi Festo Chonya alikitaka kikao hicho kitoke na majibu ya tatizo hilo,huku akiyataja baadhi kuwa ni mahudhurio hafifu na mimba na kuwa kama hayo yakidhibitiwa kunaweza kukatokea mageuzi makubwa ya kielimu katika wilaya ya Nkasi.
Alisema ni jambo lisilokubalika kuona wilaya Nkasi inashika mkia kila mwaka katika matokeo ya kitaifa katika mkoa wa Rukwa na kutaka litokee suluhisho ili kuweza kubaini chanzo cha tatizo hilo.
Naye Afisa elimu wa mkoa Rukwa Albert Mloka alisema kuwa kupitia taarifa mbalimbali za ukaguzi wamebaini kuwa Walimu wengi hawafanyi maazimio ya masomo yao hivyo maana yake ni kuwa wanaingia darasani wakiwa hawajafanya maandalizi ya somo.
Alisema kuwa kabla ya Mwalimu kuingia darasani kuna maandalizi kadhaa ya kufanya lakini wengi hawafanyi hivyo na kujikuta wakiwa waudhuriaji tu madarasani na si kufundisha kama ilivyo lengo lao na kuwa katika mazingira hayo ni vigumu kuweza kufaulisha wanafunzi.
Akitoa tathimini kwa mujibu wa taarifa alizonazo ni kuwa 50% ya Waalimu wanaingia darasani 30% ndiyo wanaofundisha na 12% ndiyo wanaofundisha kile wanachositahili kufundisha,na kuwa katika mazingira hayo ni vigumu kwa shule kuweza kufanya vizuri
Hivyo alitumia fursa hiyo kuwataka Walimu kubadilika na kufuata kanuni za ufundishaji na kuitaka idara ya elimu ya wilaya kusimama kidete kuona Walimu wanafundisha darasani na kutaka kuona sasa matokeo ya sekondari yanabadilika hasa katika msimu mpya wa masomo na kuwa sasa hataelewa kama matokeo yataendelea kuwa mabaya licha ya kutoa maelekezo hayo.
Naye Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo ambaye pia ni afisa elimu Sekondari Abel Ntupwa alisema kuwa halmashauri hiyo inatambua changamoto walizonazo wakati wao wakijitahidi kuwatatulia,huku akikemea tabia za baadhi ya Walimu kutoa kejeli kwa Wanafunzi na kudai kuwa hilo halikubaliki.
Alisema kuwa sasa hawatamuhurumia Mwalimu yeyote ambaye atabainika kuto wajibika ipasavyo kwani kuwajibika kwao kutawezesha kuondokana na aibu ya kushika mkia kila mwaka katika matokeao ya kitaifa kwa upande wa shule za sekondari.
Awali baadhi ya Waalimu katika kikao hicho walizitaja baadhi ya sababu zinazoplelekea kufanya vibaya kwa shule zao ni ukosefu wa chakula mashuleni,umbali mrefu wanakotoka Wanafunzi,ikiwa ni pamoja na mchakato unaotumika kuwapata Wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza kutokuwa na uwezo kabisa na kujiuliza walipataje nafasi ya kufaulu na kwenda sekondari wakati hawajui hata kusoma na kuandika.
Mwisho
No comments:
Post a Comment