Na Israel Mwaisaka
Nkasi
MSIMU mpya wa kilimo wilayani Nkasi mkoani Rukwa umezinduliwa rasmi huku wakulima wakipata fursa ya ya kujua mfumo mpya wa upatikanaji wa pembejeo baada ya serikali kuondoa mfumo wa vocha kwa Wakulima.
Akizungumza jana kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa msimu mpya wa kilimo kwenye soko la Wakulima la kimataifa la Isunta afisa ugani wa wilaya hiyo Samwel Mwakihaba alisema sasa pembejeo zote za kilimo zitapatikana kwa mawakala kwa bei elekezi ya serikali.
Alisema mbolea zote za kupandia na kukuzia zimepunguzwa bei ukilinganisha na miaka iliyopita ambapo sasa pembejeo zote za kilimo zitapatikana madukani kwa bei nafuu.
Alisema kuwa awali mbegu zilikuwa zikichelewa kufika lakini hivi sasa mkakati umewekwa kuhakikisha kuwa mbegu zote zinawafia mawakala kwa wakati muafaka na hakuna mkulima atakayechelewa kupanda kwa kuchelewa mbegu.
Afisa ugani huyo alisema kuwa kuanzia wiki hii ataitisha kikao cha mawakala wote wa pembejeo za kilimo ili kuona kama kila mmoja anatekeleza agizo la serikali la kuhakikisha pembejeo zote zinauzwa kwa bei elekezi ya serikali ikiwa ni pamoja na kujiridhisha kama pembejeo hizo na zinapatikana kwa wakati kwakuwa wakulima karibu waanze kilimo.
Mmoja wa mawakala wa pembejeo wilayani humo Richard Maganga yeye aliwahakikishia wakulima kuwa pembejeo nyingi za kilimo zipo na kuwataka wakulima wanaponunua mbegu kuhakikisha kuwa zina lebo ya Toxic ili kuzingatia ubora.
Baadhi ya wakulima wakizungumza gazeti hili kwenye uzinduzi huo wa msimu mpya wa kilimo wamedai kuwa wamefurahishwa na utaratibu huo uliofanywa na serikali wa upangaji bei elekezi kwa pembejeo zote lakini zaidi ni kuona kuwa pembejeo zote sasa zinapatikana kwa mawakala.
Uzinduzi huo wa msimu mpya wa kilimo uliwashirikisha watu mbalimbali ikiwa ni pamoja na makampuni mbalimbali ya pembejeo za kilimo iliwaweze kutoa elimu kwa wakulima kuhusu masuala ya kilimo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment