Na Gurian Adolf
Nkasi
SERIKALI imekubali kuipatia halmashauri ya wilaya Nkasi kiasi cha shilingi bilioni 1.5 ili kuwasaidia wananchi kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ambavyo wamejenga kwa nguvu zao.
Akizungumza jana kwenye baraza la Mamlaka ya mji mdogo wa Namanyere wilayani Nkasi mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya Nkasi Julius Kaondo alisema kutokana na uwezo ulioneshwa na Wananchi katika kujitolea kujenga vyumba vya madarasa katika vijiji vyao wao kama viongozi wa wilaya kwa kushirikiana na mkuu wa wilaya Said Mtanda waliiomba serikali kusaidia nguvu hizo za Wananchi.
Alisema kufuatia hari hiyo serikali kupitia wizara ya TAMISEMI imekubali kutoa fedha hizo ambazo zitaongezwa kwenye bajeti ya halmashauri ya wilaya ili zisaidie nguvu za wananchi ambao wameonyesha nia ya kukabiliana na uhaba wa vyumba vya madarasa.
Uongozi huo wa wilaya ya Nkasi ulitoa agizo kwa kila kijiji kijenga vyumba vitatu vya madarasa kitu ambacho kilitekelezwa na halmashauri kwa kuona kuwa ina deni kwa wananchi ikaamua kuiomba serikali kuu isaidie fedha ambazo zitatumika katika kupaua majengo hayo.
Kufuatia agizo la serikali hivi karibuni la kuhakikisha kuwa tatizo la uhaba wa madawati linaondolewa katika shule zote nchini,wilaya ya Nkasi ilijikuta imetengeneza madawati mengi lakini madarasa yakawa hayatoshi kuweza kuweka madawati hayo na kubainika kuwa kuna tatizo kubwa la vyumba vya madarasa na ndipo serikali ilipoamua kutoa agizo kwa kila kijiji kujenga vyumba vitatu vya madarasa ambalo limetekelezwa.
Sambamba na hilo mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya alisema kuwa wilaya ya Nkasi ndiyo wilaya pekee katika mkoa wa Rukwa inayorejesha asilimia 20 ya mapato katika serikali za vijiji na kuwa hadi sasa hakuna kijiji kinachoidai halmashauri fedha yoyote inayotokana na asilimia 20 kutokana na mapato ya halmashauri yanayokusanywa katika vijiji vyao.
Kikao hicho kilicho ongozwa na mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Namanyere,Isaack Chambula ambapo alimuomba mkurugenzi wa wilaya hiyo kujibu hoja mbalimbali walizokuwa nazo kwa muda mrefu na kufanya hivyo ambapo kikao hicho kilidhishwa na hatua zinazochukuliwa na uongozi wa wilaya katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment