Friday, 15 September 2017

Rc awakoromea wavuvi haramu

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Zelote Stephen ameionya idara ya uvuvi mkoani humo kuacha mzaha katika suala zima la kupambana na wavuvi haramu kwani ikifanya mzaha vizazi vijavyo vitabaki vikiwashuhudia viumbe wa kwenye maji katika picha na mikanda ya video kama katika mataifa Mengine yalivyo. 
Hayo ameyabainisha jana wakati wa zoezi  la kuteketeza zana haramu zilizokamatwa kupitia doria maalumu inayofanyika katika vijiji vya Kabwe, Isaba, Chongokatete, mandakerenge, kolwe, lupata na kisenga katika wilaya ya Nkasi ambao ni mwalo wa kijiji cha Kirando. 
Alisema kuwa kutokana na uharibifu unaofanyika wavuvi haramu hawana tofauti na vikundi vya kigaidi kama Boko Haramu na vinginevyo ambavyo havinabudi kupigwa vita na kila mpenda maendeleo ya nchi hii kwakua ni waharibifu na wauaji wa viumbe wa majini bila utaratibu. 
Mkuu huyo wa mkoa alisema haitoshi tu kuishia kukamata nyavu haramu na kuziteketeza moto bali pia wamiliki wa nyavu hizo nilazima wachukuliwe hatua Kali za kisheria.
“Kukamata na kuchoma haitoshi, kwasababu hii inaungua tu, nataka tuwachome wahalifu kwa kutumia sheria, nimechoma sana nyavu hizi na huu mtindo bado unaendelea, hii haina tija, kila tukichoma madhara yanatokea, mazingira yanaharibika, sasa tuseme basi, ningependa kusikia mhalifu kakamatwa kapelekwa mahakamani na kupewa adhabu,”
Katika kuhakikisha wahalifu hao wanapatika Zelote aliwaasa watumishi wa idara hiyo kuachana na kupokea rushwa, jambo ambalo linaonekana kukwamisha juhudi za serikali katika kulinda rasilimali zake kwaajili ya faida ya kizazi hiki na kijacho.
Alisisitiza kuwa wananchi bado wanahitaji kuendelea kupatiwa elimu juu ya umuhimu wa rasilimali hizo na wajulishwe kuwa rasilimali hizo ni za watanzania wote na hatimaye kuacha tabia ya kuvua samaki kwa zana zisizokubalika na sheria za serikali.
Mkuu huyo wa mkoa aliishauri idara hiyo kuwa panapokuwa na zoezi hilo linalofanyika mbele ya wananchi wahakikishe kunakuwa na nyavu halali zinazokidhi viwango vya serikali na kuwaelimisha wananchi tofauti ilivyo sasa ili wavuvi wasiojua wapate kufahamu matakwa ya serikali katika kuhifadhi mazingira.
Kutokana na doria hiyo iliyofanywa na kikosi cha usimamizi wa rasilimali za uvuvi Kijiji cha Kipili kwa kushirikiana na polisi pamoja na kikosi cha jeshi la wanamaji wote wa kipili kuanzia Juni hadi September 2017 waliweza kukamata nyavu zisizokidhi viwango vya serikali zenye thamani ya shilingi milioni 57.6.
Miongoni mwa nyavu zilizokamatwa ni nyavu 32 za Makira (gilinets) zenye thamani ya shilingi milioni 38.4, nyavu za dagaa zenye macho chini ya milimita 8 zenye thamani ya shilingi milioni 16.5 na makokoro ya vyandarua yenye thamani ya shilingi milioni 2.7.
Awali akisoma taarifa ya uteketezaji wa zana haramu za uvuvi kwa mgeni rasmi Afisa mfawidhi idara ya uvuvi kanda ya Rukwa Juma Makongoro alisema kuwa kuna manufaa mengi yanayopatikana kutokana na rasilimali hiyo ikiwa ni pamoja na watu kujipatia ajira, kitoweo, fedha za kigeni na kuingizia serikali kodi ambayo hutumika kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo.
Mwisho

No comments:

Post a Comment