Na Israel Mwaisaka
Nkasi
MWANAFUNZI wa Darsa la Saba Mbalu Mihangwa (15) anayesoma Shule ya Msingi Miyombo wilayani Nkasi mkoani Rukwa nusura asifanye mitihani ya kumaliza elimu ya msingi baada ya wazazi wake kumzuia ili ashiriki msiba wa mdogo wake.
Mdogo wa mwanafunzi huyo , Keneja Madirisha (8) aliyekuwa akisoma darasa la pili katika shule hiyo alifariki dunia usiku wa kuamkia siku ambayo wanafunzi wa darasa la saba nchi nzima walikuwa wakifanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi
Akisimulia mkasa huo Mwalimu mkuu wa shule hiyo Gwakisa Bisaya alisema kuwa wasimamizi wa mtihani huo walibaini kuwa Mwanafunzi mmoja hajahudhuria kwenye mtihani ndipo walipotoa taarifa kwenye uongozi wa shule na wao walichukua hatua nakuanza kumfuatilia mtoto huyo nyumbani kwao.
Alisema kuwa baada ya kufika nyumbani kwao wakiongozana na baadhi ya wasimamizi na askari Polisi walikuta msiba na baada ya mahojiano Mwanafunzi huyo alisema kuwa alizuiwa na wazazi wake asiende kwenye mtihani wa taifa ili aweze kushiriki katika msiba huo wa mdogo wake.
Alidai kuwa waliamua kumchukua Mwanafunzi huyo na kumpeleka darasani na kushiriki na wenzie kufanya mtihani huo na kuwa alifanikiwa kufanya mitihani ya juzi na jana aliendelea na mitihani hiyo ya taifa.
“tuliamua kumchukua Mwanafunzi huyo na kwa kuwa hilo lilibainika wakati wenzie wakiwa katika somo la kwanza katika mtihani huo alikimbizwa haraka kwenda kushiriki mtihani huo na kuenenda sambamba na wenzie” Alisema
Msimamizi wa mtihani huo Vitus Mwalongo alidai kuwa kilichofanyika ilikua ni kutumia nguvu kumchukua Mwafunzi huyo na baada ya kufanya mtihani huo wa kwanza mtoto huyo alikabidhiwa kwa Mwalimu mkuu ili amuhifadhi asirudi nyumbani kwao ili aweze kushiriki katika siku ya pili ya mitihani hio ya taifa na hivyo kutorudi kwao.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Ofisa elimu taaluma wa wilaya ya Nkasi George Mwahinda alidai kuwa licha ya mazingira hayo kutokea Wasimamizi wa kituo husika walichukua hatua za haraka na Mwanafunzi huyo amefanikiwa kufanya mtihani huo kwa uangalizi mkubwa na mtihani huo ukimalizika atarudishwa nyumbani kwao ili akahani msiba wa mdogo wake huyo.
mwisho
No comments:
Post a Comment