Saturday, 19 August 2017

Watumishi wa afya kuanza kulipwa mishahara

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
Katika kuboreha huduma za afya watumishi 81 wa hospitali teule za wilaya ya Nkasi na Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, zinazomilikiwa na Kanisa Katoliki  ambao mishahara yao ilisitishwa kwa zaidi ya miezi minne sasa kupisha uhakiki wa ajira zao wataanza kulipwa mishahara hiyo tena.

Waziri wa Afya Maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Ummy Mwalimu alisema hayo jana wakati akizungumza na watumishi wa hospitali ya teule ya Manispaa ya Sumbawanga ya Dr Atman (CDH) alipotembelea hospitali hiyo katika ziara yake ya kikazi mkoani hapa.

Waziri huyo alisema watumishi hao 81 walisitishiwa mishahara yao kwa kipindi chote hicho ili uhakiki wa ajira zao uweze kufanyika ambapo tayari zoezi hilo limefanyika na wataanza kulipwa mishahara hiyo mwishoni mwa mwezi huu.

"Nimewasiliana na Waziri wa Utumishi (Kairuki) kwa hiyo msiwe na shaka mishahara yenu mtaanza kulipwa kuanzia mwezi agosti na mtalipwa na malimbikizo ya miezi nyuma tangu ilipositishwa" alisema Waziri Ummy.

Awali, Maratibu wa afya Kanisa Katoliki jimbo la Sumbawanga, Sista Helena Katebela alisema watumishi hao 81 ni kati ya watumishi 151 ambao wanalipwa na serikali ambao wamekosa mishahara katika kipindi chote hicho pasipo maelezo yoyote, hali ambayo ilianza kushusha morali ya utendaji wa kazi zao za kuhudumia wagonjwa.

katika hatua nyingine, Sista Helena alisema kwamba halmashauri za wilaya za Sumbawanga, Kalambo na Nkasi zimekuwa zikisuasua kulipa fedha za mpango wa makubaliano ya huduma uliolenga kuongeza idadi ya akina mama wanaojifungulia katika vituo vya afya vinavyomilikiwa vya jimbo Katoliki Sumbawanga.

Kupitia mpango huo vituo vya afya vvinavyomilikiwa na jimbo hilo vinatakiwa kutoa huduma pasipo kuwatoza gharama wakina mama wajawazito ambapo halmashauri zinalazimika kuchangia kiasi cha Sh 10,000 kwa kila mama atakayejifungua katika kituo husika.

Sista Helena alisema katika kipindi cha mwezi julai 2010 hadi juni mwaka huu, katika vituo 11 vinavyotoa huduma hiyo kwa akina mama 12, 979 walihudumiwa ambapo madai yalikuwa jumla ya Sh milioni 129,790,000 na halmashauri hizo zimelipa Sh 36,020,000 huku deni likibaki ni Sh 93,770,000.

Alisema vema sasa halmashauri zikalipa deni hilo kwani kutolipa kwa kipindi kirefu kunafanya vituo vya afya kuelemewa kimahitaji katika kutoa huduma hali ambayo itasababisha huduma kudorora na kukwama kabisa.

Akizungumzia hali hiyo, Waziri Ummy alitaka halmashauri hizo kukaa na uongozi wa idara ya afya ya Kanisa Katoliki na kuweka utaratibu wa kulipa deni hilo haraka iwezekanavyo kwa kuwa jambo hilo limefanyika ikiwa ni sehemu ya makubaliano walioingia baina yao.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment