Na Gurian Adolf
Sumbawanga
BAADHI ya Wazazi mkoani Rukwa wameshauriwa kuacha tabia za kuamini imani za kishiriki kupita kiasi badala yake watumie hospitali na wataalamu wa afya ili waweze kupunguza vifo vinavyotokana na imani za kishirikina kwakua magonjwa mengi ya binadamu yanatibiwa hospitali.
Ushauri huo umetolewa na mganga mfawidhi wa kituo cha Afya cha Kirando Gabriel Majani wilayani Nkasi wakati akizungumza na rukwakwanza.blogspot.com ilipotaka kujua kuhusiana na ugonjwa wa ajabu ulioibuka katika sekondari ya Kirando wilayani humo ambao unawapata wanafunzi wa kike wa kidato cha tano na cha sita katika shule hiyo.
Ushauri huo ulikuja baada ya kuibuka kwa ugonjwa usiofahamika kwa baadhi ya wanafunzi wa vidato hivyo ambapo walikuwa wakipata kwikwi,kulia kwa kupiga kelele, kutetemeka mwili na kuishiwa nguvu hali ambayo ilisababisha baadhi ya wazazi hao kutaka kuwatorosha watoto wao shuleni hapo kwania ya kuwapeleka kwa waganga wajadi wakiamini kuwa wamerogwa.
Dkt Majani alisema kuwa baada ya kuwafanyia vipimo wanafunzi hao hawakubainika kusumbuliwa na ugonjwa wowote wa hatari na walipata tiba ya kisaikolojia kwakua ndilo tatizo lililokuwa likiwasumbua.
Alisema kuwa kutokana na imani hizo za jadi baadhi ya watu hufariki dunia kutokana na kuwapeleka kwa waganga wajadi ambako hakuna utaalamu wa kutibu na matokeo yake wanazidiwa na kuelemewa na magonjwa na kufariki dunia.
"wengi wa wananchi bado wanaamini imani za jadi ambazo hazina tafiti na hazitoi suluhisho la matatizo na hivyo baadhi ya wagonjwa kujikuta wakichelewa kupata matibabu sahihi na kusababisha kufariki dunia"..alisema
Kwa upande wake mkuu wa shule ya sekondari hiyo Erneo Mgina alisema kuwa wanafunzi wa kike wa shule hiyo wa kidato cha tano na sita wamekuwa wakiugua ugonjwa huo na amekua akiwapeleka katika kituo cha afya cha Kirando na wanapatiwa matibabu na kisha kuendelea vizuri na masomo yao.
No comments:
Post a Comment