Na Walter Mguluchuma
Katavi
WAKAZI mjini Mpanda mkoani Katavi wanakabiliwa na adha kubwa ya usafiri wa kufika maeneo mbalimbali baada ya wamiliki na madreva wa bajaji kuamua kufanya mgomo kwa muda usiofahamika kwalengo la kuishinikiza mamlaka ya usafirishaji wa nchi kavu na majini SUMATRA iondoe marufuku iliyoweka ya kupiga marufuku bajaji zote kufanya safari kwa kupitia barabara kuu za mjini humo.
Mwenyekiti wa waendesha Bajaji mjini humo Rashid Juma alisema wameamua kusitisha kutoa huduma ya usafiri katika Manispaa ya Mpanda na nje ya mji huo baada ya SUMATRA kupiga marufuku bajaji zote kufanya safari zake kwa kutumia barabara kuu zilizopo katika mji huo .
Alisema wameamua kusitisha huduma za usafiri kuanzia jana Agosti 7 ingawa SUMATRA lIkuwa imepatoa agizo hilo lianze kutekelezeka Agosti 8 hivyo wamesitisha huduma hiyo sio kwenye barabara kuu tu bali n'a maeneo yote hata yale ya barabara ndogo mpaka hapo itakapo waruhusu kutumia barabara kuu.
Mwenyekiti huyo alieleza kitendo cha kuwazuia kufanya safari kupitia kwenye barabara kuu kutawafanya wakose mapato na kusabisha kushindwa kulipa mapato kwenye Mamlaka ya mapato hali ambayo itawa kuwafanya madreva hao kujiingiza kwenye maswala ya uhalifu kutokana na kukabiliwa na ugumu wa maisha.
Naye mwenyekiti wa wasafirishaji ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya usalama barabarani wa Mkoa wa Katavi Nassor Arfi alisema amepata taarifa za kusimamishwa kwa huduma za usafiri wa bajaji kupita kwenye barabara kuu za Mpanda Kigoma , Mpanda Sumbawanga na Mpanda Tabora na amefanya mawasiliano na Mkuu wa Mkoa wa Katavi ambae amemwahidi kumpatia majibu baada ya kuwa amefanya mawasiliano na viongozi wa SUMATRA.
Arfi alisema mkoa wa Katavi hauna njia nyingine mbadala za kuwafanya madreva wa bajaji kutumia hivyo ni vema SUMATRA wakatumia busara ya kawaida kwenye swala hilo kulingana na mazingira yalivyo kwa sasa katika Manispaa ya Mpanda hasa wakizingatia kuwa mji huo bado ni mdogo na hauna msongamano wa vyombo vya usafiri kama miji mingine mikubwa.
Kwaupande wake meneja wa SUMATRA Mkoa wa Katavi Amani Mwakalebela alieleza kuwa nchi ya Tanzania inaendeshwa kwa kanuni na sheria na wao Sumatra wanafanya kazi kwa msingi wa sheria na kanuni na mamlaka hiyo imetumia kifungu cha18 cha sheria za usalama barabarani kuzizuia bajaji kupita kwenye barabara kuu.
Alisema pia wameangalia hali ya usalama kwa sasa baada ya barabara kuu kuwa za kiwango cha lami kumefanya usalama kwa sasa sio salama kwa bajaji kwa hivyo msimamo wa SUMATRA Mkoa wa Katavi ni bajaji zote kupita kwenye barabara ndogo na sio barabara kuu.
Mmoja wa wakazi wa mji huo Aglipina Petro alisema kuwa ameshindwa leo kumpeleka mgonjwa wake hospitali baada ya kukosa huduma ya usafiri wa bajaji huku wanafunzi na watumishi mbalimbali wakionekana kushindwa kuwahi shuleni na Katika maeneo yao ya kazi kwakua wengi wao wanatumia usafiri huo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment