Tuesday, 1 August 2017

Asakwa kwa amri ya DC

Na Gurian Adolf
Nkasi
 Mkuu wa wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, Said Mtanda ameamuru kukamatwa mara moja kwa mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kate, wilayani humo anayedaiwa kuwatoza mamilioni ya fedha wafugaji zaidi ya 50 kisha kuwaruhusu kuingiza mifugo katika kijiji hicho.
Mkuu huyo wa wilaya alitoa agizo la kukamatwa kwa mwenyekiti huyo, aitwaye Joachim Sangu juzi wakati wa mkutano wa uliofanyika kijijini hapo ambapo kuliibuka hoja ya kuwepo kwa mgogoro wa ardhi baina ya wafugaji na wakulima uliosababishwa na mwenyekiti huyo.
Katika mkutano huo wananchi wa kijiji hicho wakiwemo wajumbe wa Serikali ya kijiji, walilamikia kitendo cha Mwenyekiti huyo kushirikiana na afisa mtendaji wa kijiji ambaye amehamishwa hivi sasa ambao wanadaiwa kuwatoza kiasi cha Sh 500,000 kwa kila mfugaji na kuwaruhusu kuhamia kijijini hapo.
Kutokana na malalamiko hayo ya wananchi, mkuu huyo wa wilaya aliagiza kukamatwa kwa mwenyekiti huyo ambaye alikuwepo katika kikao hicho na kushindwa kujitetea kutokana na tuhuma hizo za kuruhusu mifugo hiyo kuingia pasipo kufuata utaratibu na kuchukua mamilioni ya fedha kutoka kwa wafugaji hao.
"Akamatwe mara moja ili uchunguzi ufanyike dhidi ya tuhuma zinazomkabili.......polisi na takukuru nawakabidhi kiongozi huyu uchunguzeni kwanini achukue fedha za kijiji na kuingiza kwenye akaunti yake ya benki" alisema Mtanda 
Awali, mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Paul James alisema kuwa wafugaji hao wapatao 50 walikaribishwa kinyemela kijiji hapo hali ambayo imeanza kusababisha kuibuka kwa migogoro ya ardhi baina ya jamii ya kifugaji na wakulima wakigombea mashamba ambayo tayari wafugaji wanadai ni sehemu ya malisho ya mifugo yao.
"Sisi tunatambua wafugaji wanne tu ndio walioingia kwa kufuata mwaka 2008, hao wengine wameingia kinyelemela baada ya mwenyekiti na mtendaji wake kuchukua rushwa ya fedha kutoka kwao...." alisema Judith Kameme ambaye ni mjumbe wa Serikali ya kijiji.
Aidha, Mwenyekiti Sangu alipotafutwa hakuwa tayari kuzungumza lolote kuhusiana na tuhuma hizo zinazomkabili.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment