Thursday, 20 July 2017

Wanawake wamwagiwa milioni 5

Na Walter Mguluchuma
Katavi
WANAWAKE mkoani Katavi wameshauriwa kujikita katika kufanya shughuli za ujasiliamali ili wawe bega kwa bega na waume zao katika kuhakikisha kuwa wanatatua changamoto mbalimbali za familia na si kukaa tu nyumbani wakiamini kuwa hiyo ni kazi ya wanaume pekee.
Ushauri  huo ulitolewa jana  na katibu wa Chama cha Mapinduzi(CCM) mkoa wa Katavi, Kajoro Vyahoroka alipokuwa akikabidhi hundi yenye thamani ya shilingi milioni tano iliyotolewa na mbunge  wa  viti  Maalumu wa  Mkoa wa  Katavi Anna  Lupembe  kwa wanachama wa   LETIC  SACOS ambayo ni ya wanawake kwa lengo la kuiongezea mtaji ili wanachama wake  waweze kujikopesha kwa wingi.
Alisema kuwa hivi sasa maisha yanazidi kuwa magumu hivyo basi ni vizuri wanawake nao wakabadirika ki  fikra badala ya kukaa tu nyumbani wakipika na kuosha  vyombo badala yake wajihusishe katika shughuli za ujasiliamali ili wachangie kipato cha familia.
Vyahoroka akizungumza katika viwanja vya ofisi ya CCM mkoa wa Katavi alisema kuwa katika kumpunguzia mahangaiko mwanaume,wanawake hawanabudi kujiunga na vikundi vya kuweka na kukopa  ili wapate mitaji itakayo wawezesha  kufanya shughuli za ujasiliamali.
Kajoro  aliwaeleza  akina  mama  hao   kuwa  fedha  hizo  wanaweza  kuziona  kuwa  ni  ndogo   lakini   endapo  fedha  hizo  wakizitumia  vizuri   zitaweza  kuwasaidia  na  kuweza  kuongeza  kipato  chao .
Aliwaambia  kuwa  fedha  watakazo kuwa wakikopeshwa wahakikishe wanazirejesha kwa wakati kwani sio msaada na kwakufanya hivyo wanachama wengine pia watapata fursa ya kukopa na hatimaye wote watapata mitaji itakayowasaidia kujikomboa kiuchumi.
Kwa upande wake Katibu  wa  SACOS  hiyo   Mawazo   Manso  alimueleza katibu  huyo wa CCM kuwa  kuwa    Sacos   hiyo imekuwa  ikidhaminiwa  na   Mbunge huyo  wa  viti  Maalumu Lupembe  ambae baada  ya kuona   Sacos   hiyo  inaanza  kulega  lega  ameamua   kuiongezea  kiasi   hicho  cha  fedha  kwaajili ya kuiongezea nguvu. 
Alisema  kuwa mpaka  sasa  ina jumla   ya  wanachama  75 ambapo   hapo   awali  walikuwa  60  na   wanachama  15  wamejiunga  mwezi  huu  na   mpaka sasa   Mbunge  huyo   amesha  toa   kiasi  cha  shilingi   Milioni 45  kwani  awali  alikuwa ameipatia  kiasi  cha   shilingi  milioni  40.
Alifafanua  kuwa kabla  ya  kupewa  fedha  hizo   wakinamama   hao  wanaounda   Sacos  hiyo   waliaandaliwa   mafunzo na ya   ujasiliamali  yaliyofanyika  kwa   muda wa  siku   sita na  walifundishwa  na   mkufunzi  kutoka   Dares  salaam ambaye aliwajengea uwezo katika masuala ya biashara.
Naye Mwenyekiti wa  Sacos   hiyo Maria  Futakaba   alisema  kuwa hivi sasa   wanaotunza   familia  ni   wakina   mama   hivyo   endapo   fedha  wanazopewa  wakizitumia  vizuri   zitasaidia kwenye  familia  zao  kwa  kuweza  kusomesha  watoto  na  pia  kuwa  na  familia  yenye  afya  nzuri.
Aliwasihi wanawake hao kuwa waaminifu ili wasimvunje moyo mbunge huyo kwani yupo kwaajili ya kuwasaidia kwakua walimchagua naye aliahidia kuwatumikia.
Mwisho

No comments:

Post a Comment