Monday, 17 July 2017

Wakazi wa kata ya Majengo wakerwa na kuzagaa kwa mifugo

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
WANANCHI wa kata ya Majengo Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa wamelalamikia kitendo cha kuzagaa kwa mifugo ya aina mbalimbali ikiwemo mbwa ambapo wameiomba idara ya mifugo kuhakikisha inadhibiti suala hilo kwani limekuwa  kero katika eneo hilo.
Mbunge wa jimbo la  Sumbawanga Aesh Hilary akiwahutubia wakazi wa Majengo

Malalamiko hayo walitatoa jana mbele ya mbunge wa jimbo  la  Sumbawanga mjini Aesh Hilary alipokuwa katika siku ya tatu ya  ziara yake ambapo anafanya  ziara ya kutembelea katika jimbo hilo akiwa na wataalamu mbalimbali wa halmashauri hiyo wakijibu kero za wananchi wa jimbo la  Sumbawanga mjini.
Akiwa katika kata ya Majengo mjini Sumbawanga wananchi wa eneo hilo walilalamikia kitendo cha kukithiri kuzurula kwa mifugo mbalimbali na hasa mbwa ambao wamekuwa ni tishio kwa usalama wa wakazi hao.
Mmoja wa wakazi hao Issa Katembo alisema kuwa mbwa hao wamekuwa wengi na wanatembea kwa makundi hali ambayo ni tishio kwa usalama  wao na hasa  watoto wadogo pindi wanapokwenda mashuleni nyakati za asubuhi.
Meya wa manispaa ya Sumbawanga Justine  Malisawa  akiwahutubia wakazi wa kata ya majengo

Alisema kuwa kibaya  zaidi iwapo utazuka ugonjwa wa kichaa cha mbwa kwani huenda mbwa hao wakaanza  kuuma watu hovyo  na kuwaambukiza ugonjwa huo hivyo kuiomba idara ya mifugo kuanza operesheni ya kuwaua kwa kuwapiga risasi ili kuwapunguza  kwani wanaonekana wamekuwa wengi kuliko hata mbuzi ambao wanafugwa kwaajili ya kitoweo katika eneo hilo.
Naye Bora Mohammed Amour mkazi wa eneo hilo la kata ya Majengo alilalamikia huduma duni  na majibu mabaya ya watendaji wa afya kata hiyo ambapo alisema kuwa yamekuwa  yakiwaudhi wagonjwa na kuwakatisha tamaa kiasi kwamba kuamua kwenda kutafuta matibabu katika kata nyingine ambapo watumishi wake wanaheshimu maadiri ya taaluma yao.
Wakazi wa kata ya majengo wakiwa katika mkutano wa hadhara katika kata hiyo

Alisema kuwa wapo baadhi ya watumishi wa idara ya afya ambao wanafanya  kazi katika maeneo ya kata hiyo wanakera kwa kauli zao na kutojali kuhudumia wagonjwa kwa upendo kana kwamba wamelazimishwa kufanya kazi hiyo.
Kwa upande wake mbunge Hilary aliwashukuru wananchi wa kata hiyo kujitokeza katika mkutano huo na kueleza kero zao na kuwasihi watendaji wa halmashauri hiyo kuzifanyia  kazi kero hizo ili kuzimaliza kwani nia ya serikali ya awamu ya tano  ni kuona wananchi wakiishi kwa amani  na furaha huku wakifanya  kazi zao za ujenzi wa taifa.
Mwisho

No comments:

Post a Comment